Mfamasia kutoka Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Frank Milanzi akikagua na kupanga baadhi ya vifaa tiba vilivyonunuliwa kwa ajili ya majeruhi wa ajali ya moto kabla ya kukabidhiwa kwa uongozi wa Mkoa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akizungumza wakati wa kukabidhi misaada ya vifaa tiba kwa majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro eneo la Msamvu na kusababisha vifo vya watu 95. Katikati ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bw. Noel Kazimoto na wa mwisho ni Bw. Twalib Muzakir Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Akitambulisha aina ya vifaa tiba vilivyonunuliwa kwa majeruhi wa ajali ya moto ni Dkt Bunini Manyilizu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya ya Chuo Kikuu Mzumbe, wakati ya hafla ya kukabidhi vifaa tiba vilivyotolewa na Chuo hicho kutibu majeruhi wa ajali ya Moto. Wakishuhudia tukio hilo ni Bi. Prakseda (aliyeshika kipaza Sauti) kutoka TBC, akifuatiliwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka (katikati mwenye tai).
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka (kushoto mwenye suti) akipeana mkono na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirya Ukio baada ya kubabidhi vifaa tiba kwa majeruhi wa ajali ya moto. Katikati ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bw. Noel Kazimoto.

*****************



Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, leo kimekabidhi misaada ya vifaa tiba kwa ajili ya majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro Jumamosi ya tarehe 10 Agosti 2019 na kusababisha vifo vya watu 95.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo; Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Lughano Kusiluka amesema, Jumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe wamechangia vifaa tiba vya thamani ya Tshs. 6,343,000/- vikijumuisha madawa, sindano, dripu, gozi za vidonda, madawa ya maumivu, maji, taulo za kike na madawa mengine baada ya kuonekana uhitaji mkubwa wa vifaa hivyo kufuatilia hali ya majeruhi na matibabu wanayoendelea kupatiwa kwenye hospitali hiyo.

“ Vifaa tunavyokabidhi ni michango ya watumishi, wanafunzi na Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwakuwa na sisi tumeguswa na tukio hili, ni sehemu ya wananchi wa Morogoro hivyo hatuna budi kujitoa kwa hali na mali kuokoa Maisha ya wenzetu. Tunatamani kuona majeruhi wa ajali hii wanatibiwa na kurejea kwenye afya zao” alisema.

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo; Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amesema; Serikali ya Mkoa imefarijika sana kwa namna Chuo hicho kilivyojitoa tangu ajali hiyo ilipotokea kwa msaada wa haraka wa gari la Wagonjwa kuwakimbiza hospitali ya Rufaa Muhimbili na walivyojitoa kuchangia damu kabla ya msaada wa vifaa walivyokabidhi leo.

“ Tunawashukuru sana Uongozi na Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa michango yenu kwa hakika haitawasaidia majeruhi wa ajali hii tu lakini na wagonjwa wengine wenye uhitaji na hasa kwa kuzingatia Mkoa wetu uko katikati na hivyo kuwekuwa na wajeruhi wengi wa ajali ambao wanahitaji msaada wa haraka wanapofikwa na majanga kama haya” alisisitiza.

Amewataka kuendelea kujitoa kwa wananchi wa Morogoro kila inapobidi kufanya hivyo kwakuwa uwepo wao ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya Wananchi.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kusirya Ukio ameeleza hali ya majeruhi wa ajali ya moto ambapo hadi kufikia leo idadi yao ni 17 (kumi na saba) wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa na kati yao baadhi wameanza kufanya mazoezi.

Hata hivyo matibabu yao bado yatachukua muda mrefu kutokana na aina ya majeraha waliyoyapata, hivyo misaada bado inahitajika vikiwemo vifaa tiba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...