Na Mwandishi Wetu Mwanza

Marekebisho ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Namba 3 ya Mwaka 2019 yameweka bayana mipaka ya Mashirika yanayofanya shughuli za kijamii na kiuchumi kutekeleza takwa la kisheria la kujisajili chini ya Sheria Namba 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa mabadiliko ya Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali Na. 3 ya mwaka 2019, na kwamba muda wa kukamilisha usajili huu ni miezi miwili kuanzia tarehe 1 Julai, 2019.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Mkoani Mwanza Msemaji wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Mendelee ya Jamii) Bw. Erasto Ching’oro ameeleza kuwa NGOs zilizosajiliwa awali chini ya Sheria nyingine zinatakiwa ziwe zimejisajili chini ya Sheria ya NGO mapema kabla ya kukamilika kwa miezi miwili ya takwa la kisheria

Zoezi la Usajili linaendelea katika Kanda ya Ziwa kwa mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera kwa muda wa siku tatu na utaanza kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 10 Agosti, 2019 katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. 

Bw. Erasto amesisitiza wadau kujitokeza kwa wingi katika siku zote za zoezi la usajili kwa lengo la kukamilisha zoezi la kuhamisha usajili katika muda elekezi wa miezi miwili kuanzia tarehe 1 Julai, 2019 ili kuepuka usumbufu hivyo kupata uhalali wa kuendelea na shughuli za shirika.

Ameongeza kuwa, walengwa wakuu wa Usajili unaoendelea ni Mashirika na Taasisi zinayofanya kazi za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya jamii, ambao awali walisajiliwa chini ya Sheria nyingine ikiwemo Sheria ya Vyama Sura 337, Sheria ya Udhamini Sura 375, na Sheria ya Makapuni Sura 212/213, kama zilivyofanyiwa mabadiliko na Sheria Namba 3 ya mwaka 2019, na sasa wanatakiwa kusajiliwa chini ya Sheria stahiki ikiwemo Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Namba 24 ya mwaka 2019 ili kuhuisha taarifa za NGOs na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ngazi za utendaji.

“Sheria hii inayataka Mashirika yote yaliojisajili chini ya Sheria nyinginezo kuhakikisha kuwa yamekamilisha uhamisho wao ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia siku ya tarehe 1 Julai, 2019 ili kuendelea kupata haki na hadhi ya kuendesha shughuli zao katika jamii kwa kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni. Alisisitiza Bw.Erasto

Aidha, Bw. Erasto ameongeza kuwa zoezi la kuhuisha usajili wa mashirika yanayofanya kazi za kijamii na kiuchumi katika ngazi ya jamii hapa nchni lina umuhimu ukubwa kwani litawezesha kuwa na matumizi bora ya rasilimali za nchi kwa kuwa na mgawanyiko wenye uwiano wa afua mbalimbali katika kuhudumia jamii, jamii itahamasishwa kuchangia maendeleo yao, itakuza ajira na kuongeza weledi katika utekelezaji wa miradi na kukuza uwazi na uwajibikaji. 

Usajili huu unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kisheria linaloelekeza Mashirika na Taasisi zote zinazofanya kazi za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi kuhakikisha kuwa yamekamilisha usajili wake chini ya Sheria Namba 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa mabadiliko chini ya Sheria Namba 3 ya mwaka 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...