NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO.

SHULE ya msingi Kizuiani,kata ya Kisutu,Bagamoyo mkoani Pwani inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 16 hali inayosababisha wanafunzi kusoma kwa awamu ili kuondoa mlundikano madarasani pamoja na shule kukosa hati miliki.

Aidha walimu shuleni hapo hawana vyoo ambapo hulazimika kutumia choo cha nyumba ya mwalimu karibu na shule hiyo.

Akitoa taarifa ya shule ya msingi Kizuiani,kwa mbunge wa jimbo la Bagamoyo dkt.Shukuru Kawambwa ambae alikwenda kuzungumza na walimu katika muendelezo wa ziara yake ya jimbo, kaimu mwalimu mkuu Joseph Ludovick alisema ,kwa sasa kuna jumla ya wanafunzi 1,170 ,vyumba vya madarasa 12 ambavyo havikidhi mahitaji.

"Kuna darasa ambalo linaongezwa kujengwa lakini bado itakuwa haitoshi kutokana na idadi ya wanafunzi na madarasa yaliyopo ,na ndio maana tuliona wasome kwa awamu ili kuondokana na mlundikano wa wanafunzi darasani"alifafanua Ludovick.

Ludovick alieleza, pia walimu wanalazimika kwenda kujisaidia katika choo cha nyumba ya mwalimu shuleni hapo, lakini wanamshukuru mbunge wa jimbo hilo ,dkt Shukuru Kawambwa kwa kuwawezesha kuanza kujenga choo ambacho kipo hatua ya chini.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni, upungufu wa matundu ya vyoo 38, uzio,meza na viti kwa ajili ya ofisi ya walimu na upungufu wa nyumba za walimu 26 kwani iliyopo ni moja.

"Licha ya changamoto hizo lakini tumefanikiwa kumaliza tatizo la madawati na kuinua taaluma "alijieleza.Ofisa elimu kata ya Kisutu, Yusuph Salim alisema, kama kata wamechukua hatua ya kujenga darasa moja ambalo lipo hatua ya gebo hivyo wanaomba wadau na wahisani kujitokeza kusaidia liweze kukamilika.

Nae Kawambwa alisema, ataendelea kushirikiana wadau wa elimu na kamati za shule jimboni humo, kuboresha sekta ya elimu ili kupunguza na kutatua changamoto zilizopo kulingana na uwezo uliopo.

Kawambwa aliutaka, uongozi wa shule hiyo kufuatilia eneo jingine ambalo litasaidia kuanza kujenga shule nyingine -Kizuiani B ambapo wanafunzi wengine waweze kupunguzwa endapo itakuja kukamilika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...