Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Joelson Mpina ( katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo Prof.Elisante Ole Gabriel (kulia) na Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi binafsi ya TRADEMARK East Africa baada ya majadiliano yenye lengo la kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya serikali kwa njia ya kielektroniki yaliyofanyika Wizarani jijini Dodoma leo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo) Profesa Elisante Ole Gabriel( katikati) akiongea na wataalam na wawakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi( hawapo pichani) kwenye kikao cha kujadili uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali  kwa kuahirikiana na Trademark East Africa kwenye ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mtumba jijini Dodoma leo. (19/8/2019)

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.Elisante Ole Gabriel amezitaka taaisisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielekroniki ili kuweza kutoa gawio serikalini.

Katibu Mkuu Prof.Gabriel ameyasema hayo jijini Dodoma leo (19.8.2019) wakati akifungua kikao cha majadiliano kati ya wataalamu wa sekta za Mifugo na uvuvi na wataalam kutoka taasisi binafsi ya Trade Mark East Africa yenye lengo la kusaidia uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia ya kielekroniki.

Prof.Gabriel alisema kuwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali ni kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli katika jitihada zake za kuinua uchumi na kuleta maendeleo nchini.

Akitolea mfano wa upotevu wa mapato ya serikali hususan kwenye Sekta ya Mifugo, Prof.Gabriel alisema kwenye mnada wa Maswa ulikuwa ukikusanya kiasi cha Shilingi 756,000 kwa siku lakini baada ya kuweka udhibiti kwa kupeleka wasimamizi mapato yaliongezeka na kufikia shilingi 7,028,000 kwa siku.

Kwa upande wa mnada wa Halmashauri ya Bariadi,mkoani Simiyu,Prof.Gabriel alisema baada ya udhibiti mapato yaliongezeka kutoka shilingi mil.2.5 hadi mil. 3 kwa siku na kufikia shilingi 14,950,000 kwa siku.

Aidha Katibu Mkuu aliwataka wataalam hao baada ya kuwa na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato, pia kufikiria na kuona njia nyingine za kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato, akitolea mfano utalii kwenye sekta za Mifugo na Uvuvi nchini.

Prof.Gabriel aliiahidi taasisi hiyo yenye makao yake makuu jijini Nairobi nchini Kenya kuwa Wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kufanikisha azma hiyo ya kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.

Kabla ya kumalizia na kuashiria ufunguzi rasmi wa kikao kazi hicho, Prof.Gabriel alisisitiza suala la elimu kwa umma kuhusu matumizi ya mifumo hiyo kuwa ni muhimu sana kutolewa hususan kwa wafugaji na wavuvi ambao ndio wadau wakuu wa sekta za mifugo na uvuvi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi hiyo nchini, Bw.John Ulanga alimshukuru sana Katibu Mkuu na wataalamu wake kwa kuonyesha utayari wa kushirikiana nao na kusema haijawahi kutokea katika taasisi zote walizofanya nazo kazi kuona utayari na ushirikiano kama walioupata kwa wizara ya mifugo na uvuvi.

Ili kufanikisha azma hiyo.Bw.Ulanga alisisitiza kuwepo na utayari wa kubadilika fikra katika utendaji ndani ya Wizara na taasisi zake vinginevyo mifumo hiyo haitakuwa na faida yoyote.

Wakichangia hoja wakati wa uwasilishwaji wa mada kutoka taasisi binafsi ya Trade Mark East Africa wataalam wa wizara ya mifugo waliipongeza taasisi hiyo na kuitaka kujitahidi kutumia changamoto walizokutana nazo kwenye taasisi nyingine kuboresha mifumo ya wizara ili kurahisisha matumizi ya mifumo hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Sekta ya Mifugo, Bw.Amosy Zephania akihitimisha kikao hicho aliishukuru taasisi hiyo kwa kuonyesha nia ya kuisaidia wizara na kuahidi ushirikiano wa hali ya juu.

Alisema kwa kuwa wizara ilishaanza mchakato wa kuwa na mifumo hiyo basi ni vema taasisi hiyo ikashirikiana kwa haraka ili kufanikisha malengo ya wizara ya kuokoa fedha nyingi zinazopotea kwa kukosekana kwa mifumo ya udhibiti wa ukusanyaji mapato ya serikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...