Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya uwakala wa huduma za kibenki na Shirika la Posta nchini ili kupanua wigo wa huduma za benki hiyo sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa maeneo ya vijijini.

Hatua hiyo inatajwa kuwa itaongeza wigo wamtandao wa utoaji huduma za kifedha kwa njia ya kijiditi huku ikienda sambamba na azma ya serikali ya kupanua ushiriki wa wananchi katika shughuli za kifedha (financial inclusion).

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa kutoa huduma za kubeki kati ya Posta na NBC jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema kupitia mtandao wa ofisi za Shirika la Posta nchini lenye mtandao wa matawi 370, kutaiwezesha Benki ya NBC kuwafikia maelfu ya wananchi nchi nzima katika utoaji wa huduma zake za kibenki kwa gharama nafuu.

“Ushirikiano huu kati ya NBC na Posta utawezesha ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya serikali kwa urahisi zaidi. Kwani ulipaji wa kodi na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yatafanyika katika mazingira salama na rafiki kwa wananchi kupitia ofisi za Posta. Wafaidikaji wa ushirikiano huu kati ya NBC na Posta sio tu wateja bali watakuwepo wastaafu, wanafunzi, wakulima, wazazi, na wafanyabiashara.’’ Alisema

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema ushirikiano huo utawawezesha kutumia mifumo ya kidijitali na wingi wa ofisi za posta katika kutoa huduma za kibenki nchi nzima.

“Kwa sasa NBC ina mawakala wapatao 2,000 na hivyo kuungana na Shirika la Posta, kupitia mtandao wa ofisi zake 370, kutatuwezesha kuongeza idadi ya wananchi watakaofikiwa na huduma za kibenki kwa ukaribu.’’ alisema

Aliongeza kuwa ushirikiano huo, ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali kwa mabenki ya kupeleka huduma ya kifedha kwa wananchi hasa walioko mikoani na vijijini. Kwa upande wake Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang'ombe alisema kwa kuanza shirika hilo na NBC wataanza kutoa huduma katika ofisi 99 zilizo maeneo mbalimbali nchini.

“Huduma hizi ni zile zote za kibenki, kukusanya mapato ya serikali, kuhamisha na kutuma fedha, kufungua akaunti pamoja na huduma nyingine za kibenki.

“Katika kuimarisha shirika kibiashara na kurahisisha wananchi wapate huduma kwa ukaribu shirika tayari linashirikiana taasisi kadhaa ikiwemo Benki ya Posta, Necta, MSD, Tanesco, NIC, mifuko ya hifadhi ya jamii, mashirika na makampuni mbalimbali,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta nchini Luteni Kanali Mstaafu Dk. Haroun Kondo alisema kulingana na mageuzi ya kimfumo na maboresho mbalimbali yanayofanywa sasa na shirika hilo, yatatoa nafasi bora kwa taasisi na makampuni mbalimbali kuvutiwa kuweka ofisi au kuingia ubia wa kutoa huduma au uwakala wa huduma zake.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Luteni Kanali Mstaafu Dk. Haroun Kondo (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kushoto) wakifurahia uzinduzi wa uwakala wa huduma za kibenki kati ya Shirika la Posta na NBC ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa maeneo ya vijijini. Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) na Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang'ombe (kushoto) wakisaini mikataba ya ushirikiano katika utoaji huduma za kubeki kati ya Shirika la Posta na Benki ya NBC ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa maeneo ya vijijini.
Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) na Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang'ombe (kushoto) wakionesha mikataba ya makubaliano ya utoaji huduma za kubeki kati ya Shirika la Posta na NBC ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa maeneo ya vijijini. Anaeshuhudia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati). Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) na Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang'ombe (kushoto) wakijipongeza mara baada ya kusaini mikataba ya makubaliano ya utoaji huduma za kubeki kati ya Shirika la Posta na Benki ya NBC ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa maeneo ya vijijini. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...