Charles James, Michuzi TV

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amelipongeza Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa kwa namna ambavyo wamekua mstari wa mbele katika kusaidia Jamii kimwili na kiroho.

Spika Ndugai ameyasema hayo wakati akizindua rasmi kampeni ya uchangiaji ujenzi wa wodi ya Mama na Mtoto pamoja na ununuzi wa vifaa tiba kwenye kituo cha afya cha St Luke kinachomilikiwa na Kanisa hilo.

Amesema Kanisa la Anglikana limekua mstari wa mbele katika kusaidiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi na kuwataka wadau mbalimbali kuungana na Kanisa hilo kwa kuwachangia ili waweze kufanikisha ujenzi huo ambao utakua na manufaa kwa wanampwapwa na watanzania kwa ujumla.

" Nichukue fursa hii kulipongeza sana Kanisa, nyinyi mmekua mstari wa mbele haswa kufanya kazi za kitume pamoja na za kijamii. Haya ndio mambo ambayo tumeagizwa na Mwenyezi Mungu kuyafanya na kuyasimamia duniani.

Nitoe wito kwa serikali, mashirika binafsi na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Nchi kuunga mkono maono haya ya kanisa katika kuboresha huduma za afya na hasa tunapowaona wakiwa na mawazo makubwa ya kujenga Hospitali kubwa," amesema Spika Ndugai.

Nae Askofu Mkuu wa Dayosisi hiyo ya Mpwapwa, Dk Jacob Chimeledya amemshukuru Spika Ndugai kwa kukubali kushiriki katika kampeni hiyo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza ili kukamilisha kiasi hicho cha Shilingi Milioni Mia Sita.

Amesema kituo kina uhitaji mkubwa wa ongezeko la uwezo wa kulaza wagonjwa ili kukidhi mahitaji yaliyopo huku wakilenga kuongeza vitanda 40 ili viwe 60 sawa sawa na mahitaji.

" Tunaomba wadau na Serikali watuunge mkono katika azma yetu hii ya kujenga wodi mpya ya kisasa kama inavyoelekezwa na Wizara ya Afya kwani kufanya hivyo ni kuunga mkono juhudi kubwa inayofanywa na Mhe Rais Dk John Magufuli katika kuboresha sekta hii ya afya," Amesema Dk Chimeledya.

Kituo hicho cha afya pia kinatoa huduma za kiliniki tembezi kwenye vijiji vya Bumila, Mang'hangu, Lupeta, Makutupa na hapo awali Iyoma na Idilo.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Job Ndugai akizungumza katika viwanja wa Nyerere jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uchangiaji ujenzi wa Kituo cha Afya wilayani Mpwapwa.
 Spika wa Bunge, Mhe Job Ndugai (katikati) akiongoza matembezi ya uchangiaji mfuko wa upanuzi wa kituo cha afya cha St Luke kilichopo wilayani Mpwapwa kinachomilikiwa na Kanisa la Anglikana. Kulia ni Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa, Dk Jacob Chimeledya.
Baadhi ya wananchi na wadau wa afya wakiwa kwenye matembezi ya uchangiaji upanuzi wa ujenzi wa kituo cha afya cha St Luke kilichopo wilayani Mpwapwa. Matembezi hayo yaliongozwa na Spika wa Bunge, Mhe Job Ndugai

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...