MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevitaka vyombo vya habari viwili viombe radhi kwa siku saba mfululizo kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni) ikiwemo kuonesha na kuchapisha picha mbalimbali za ajali ya gari la mafuta, iliyotokea Msamvu, Morogoro.

Kamati ya Maudhui ilitoa onyo hilo kwa Lemutuz Online Tv na Global Tv ambapo wametakiwa kuomba radhi kuanzia Septemba 4 mwaka huu.

Akisoma uamuzi huo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Valeria Msoka alisema katika ajali iliyotokea Agosti 10 mwaka huu baadhi ya vyombo vya habari hususan Online TV zaidi ya 15 zilichapisha na kuonesha picha za miili ya watu wakiofariki katika ajali hiyo kinyume cha sheria, kanuni na maadili ya uandishi na utangazaji wa habari.

Alisema baadhi ya vyombo hivyo viligundua makosa yao na kuziondoa picha hizo na kwamba Lemutuz Online Tv na Global Tv walishindwa kujirekebisha na Agosti 28 mwaka huu walifika mbele ya kamati hiyo na kujieleza.

"Katika utetezi wao Lemutuz Online Tv ilieleza kuwa kosa hilo lilisababishwa na uzembe wa msimamizi wao wa maudhui ambaye hakutumia busara na kuzingatia weredi katika uchapishaji video ile,Global Tv ilisema ilichukua tahadhari kubwa ya kuziziba picha za miili ya watu waliokuwa wameungua katika ajali ile kwa kuweka vivuli lakini ilitokea tatizo la kiufundi na kuonesha picha hizo chini ya kivuli,"amesema Msoka

Ameongeza kuwa vyombo vyote hivyo vya habari vilikiri makosa yao na kuomba radhi na kuahidi kutorudia tena na baada ya kusikiliza kwa kina maelezo ya utetezi wao, kamati imeona imekiuka kanuni za mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (maudhui mtandaoni) ya mwaka 2018.

Msoka amesema, kutokana na hilo kamati ya maudhui imeamua kutoa onyo kali na kuamuru chaneli hizo mbili kuomba radhi kwa watazamaji kupitia chaneli zao kwa siku saba mfululizo kuanzia Septemba 4 mwaka huu.

Amesema imeshauri chaneli zote mbili kuimarisha usimamzi makini wa chaneli zao ili kuhakikisha maudhui yao ni salama kisheria na kimaadili kabla ya ya kuwekwa mtandaoni.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo imetoa onyo kali kwa Televisheni ya East Africa (EATV) kwa kurusha maudhui yasiyo na maadili Julai 2 mwaka huu kupitia kipindi chake cha 'Dadaz' kipengele cha Mtukati.

Pia ilitoa onyo kali kwa kituo cha TBC FM Radio , kwa kukiuka agizo la serikali la kutosoma habari za magazeti kwa undani.

Alisema radio hiyo ilitenda kosa hilo kupitia kipindi chake cha 'Busati' kipengele cha magazeti ambapo mtangazaji wa kipindi alisoma kwa undani habari mbalimbali zilizoandikwa katika magazeti ya uhuru na Habari Leo.

Alisema vyombo vyote vya habari viligundua nakukiri makosa yao na kuomba radhi ambapo kamati imevishauri kuimarisha na kuboresha usimamizi, utayarishaji na utangazaji wa vipindi vyao.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...