Na. Catherine Sungura- Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesaini mkataba wa makubaliano wa miaka mitatu na serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kuimarisha afya ya msingi nchini.

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainabu Chaula alisema kuwa wizara yake imesaini mkataba huo na serikali ya Ujerumani katika kuboresha sekta ya afya katika maeneo manne ambapo sekta hiyo itapata kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 26.6.

Dkt. Chaula amesema kwamba kwa mwaka huu wameweka makubaliano ili fedha hizo zitolewe kwa wakati mmoja na kuweza kutumia mfumo wa Force Akaunti kama walivyoweza kutumia kwenye ujenzi wa Vituo vya afya na Hospitali za Wilaya na Mikoa katika kuboresha sekta ya afya nchini.

“Tumeanza mahusiano tangu mwaka 1961, kuanzia mwaka 2003 huu ni mkataba wa tano na mkataba wao ni wa miaka mitatu mitatu ambapo umejikita katika kuimarisha afya ya msingi katika halmshauri zetu katika vituo vya afya pamoja na zahanati”.

Dkt. Chaula alitaja maeneo yatakayonufaika na mkataba huo ni uhimarishaji wa taarifa, afya ya mama na mtoto, uzazi wa mpango, bima ya afya kwa akina mama wajawazito pamoja na utawala bora jinsi ya kutumia fedha hizi kulingana na kanuni na taratibu za nchi.

“Huu ni muendelezo wa mkataba wa miradi mingi ambayo tumeifanya katika kuboresha sekta ya afya, kama mnavyokumbuka hadi sasa hivi tumeshafanyia ukarabati wa vituo vingi vya afya ambapo tuna vituo 470 ambavyo vimeshafanyiwa ukarabati tangu mwaka 2017 katika ngazi za zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya.

Aidha, Dkt. Chaula alisema Serikali iliwekeza shilingi bilioni mia moja na milioni mia tano katika hospitali za halmashauri.

“Zamani hawa wenzetu walikua wakitumia wakandarasi wao na pesa wanakaa nazo hivyo tumekaa nao na kukubaliana kama fedha hizi watazitoa kwa wakati mmoja ili tuweze kuzisimamia kama tulivyofanya kwenye vituo tulivyoanza ili kuweza kutekeleza kwa umakini na kupata matokeo makubwa katika kipindi hiki” . Amesema Dkt. Chaula. 

Kwa upande wa hali ya uzazi, mama na mtoto Katibu Mkuu huyo alisema hivi sasa inakaribia asilimia 80 ya akina mama wajawazito wanajifungulia kwenye vituo vya afya tofauti na zamani ambapo kulikuwa na changamoto kubwa kwani wengi walikua wanajifungulia majumbani kwa asilimia 39 na kufuatia na asilimia 59 hii ni kutokana na kuboreshwa kwa vituo vya afya pamoja na mikakati mbali mbali ya kuhakikisha akina mama wote wanajifungulia kwenye vituo vya afya.
 Mwakilishi Mkazi wa Shirika la giz Dkt. Mike Falke akisaini mkataba wa makubaliano na serikali ya tanzania kupitia wizara ya afya katika kuimarisha afya ya msingi nchini, kushoto ni katibu mkuu wa wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula
 Katibu Mkuu Idara kuu Afya Dkt. Zainabu Chaula akisaini mkataba huo wa shilingi bilioni 26.6 kutoka Serikali ya Ujerumani,halfa hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa wizara uliopo mji wa serikali Mtumba.
 Viongozi hao wakibadilishana mikataba hiyo mara baada ya kusaini
Mwakilishi wa Serikali ya Ujerumani.Bi. Vera Rosendahl akizungumza wakati wa kusaini mkataba kati ya nchi yake na Serikali ya Tanzania
Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akimuonesha kitabu cha masuala ya mama na mtoto Bi. Vera  Rosendahl mwakilishi kutoka Serikali ya Ujerumani

Viongozi wa Wizara na serikali ya Ujerumani wakati wa mazungumzo ya pamoja katika kuboresha sekta ya afya
 Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula na baadhi ya viongozi wa  giz na serikali ya Ujerumani mara baada ya kusainiana mkataba

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...