Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisalimiana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi Sarah Cooke mara baada ya kuwasili katika ofisi ndogo za wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam kwa ajili ya mazungumzo ya kikazi leo tarehe 2 Octoba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi Sarah Cooke katika na ujumbe wake mara baada ya mzungumzo ya kikazi katika ofisi ndogo za wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo tarehe 2 Octoba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Mtendaji mkuu wa kampuni ya kutengeneza mitambo ya kubangua korosho ya Oltremare ya nchini Italia Ndg Stefano Massari katika ofisi ndogo za wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo tarehe 2 Octoba 2019. Wengine pichani ni Dkt Maurizio Papaleo kutoka kampuni ya Oltremare na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya T Masasi Agro Bi Sarah Masasi
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji mkuu wa kampuni ya kutengeneza mitambo ya kubangua korosho ya Oltremare ya nchini Italia Ndg Stefano Massari katika ofisi ndogo za wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo tarehe 2 Octoba 2019. Wengine pichani ni Dkt Maurizio Papaleo kutoka kampuni ya Oltremare na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya T Masasi Agro Bi Sarah Masasi


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 2 Octoba 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi Sarah Cooke katika ofisi ndogo za wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Kilimo Mhe Japahet Hasunga ameeleza kuwa mazungumzo hayo yalijikita zaidi kwenye namna ya kuimarisha zaidi mahusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ambayo yanaendelea kudumu na kuwa na mafanikio makubwa.

Majadiliano hayo yamehusu pia miradi mbalimbali mahususi ambayo inaweza kuibuliwa kwa pamoja na kushirikiana wa pamoja ili kufikisha adhma ya serikali ya awamu ya tano kuwa na maendeleo endelevu kupitia sekta ya viwanda.

Pia majadiliano hayo yalijikita kwenye upanuzi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero Mkoani Morogoro kwani moja ya kampuni za Uingereza ni wawekezaji katika kiwanda hicho.

Alisema kuwa dhamira ya majadiliano ya kiwanda hicho cha sukari ni kuona namna ya kuongeza uzalishaji mara dufu ya huu wa sasa.Kadhalika, katika majadiliano hayo Waziri Hasunga amesema kuwa wamezungumzia namna ya kuondoa vikwazo vya mashirikiano na vya kufanya biashara au kufanya uwekezaji nchini na hususani vile ambavyo serikali ya Tanzania imeviweka katika mkakati wa kuondoa dosari na vipingamizi katika kufanya biashara nchini vijulikanavyo kama “Blue Print”.

Pia majadiliano kuhusu namna ambavyo serikali imeamua kuja na sera mpya ya kilimo ya mwaka 2019 na namna ambavyo sheria itatungwa hivyo kupelekea kuwa na sheria ya kulinda kilimo itakayokuwa na vipaumbele mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi Sarah Cooke amesema kuwa mkutano wake na Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga umekuwa na mafanikio makubwa ukiwa na mtazamo wa mbali wa kuendeleza sekta ya kilimo.

Cooke alipongeza mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Serikali ya Tanzania katika sekta ya Ardhi kwa kipindi kifupi. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili ASDP II.

Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kutengeneza mitambo ya kubangua korosho ya Oltremare ya nchini Italia Ndg Stefano Massari.

Mhe Hasunga amesema kuwa Mtendaji mkuu wa kampuni ya kutengeneza mitambo ya kubangua korosho ya Oltremare ya nchini Italia Ndg Stefano Massari kwa ushirikianio ya wazawa amemuahidi kuleta mitambo ya kisasa ili kujenga kiwanda kikubwa ambacho kitakuwa na uwezo wa kubangua Tani 30,000 kwa mwaka.

Amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utapelekea kufikia lengo la serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuhakikisha kuwa korosho zote zinazozalishwa zinabanguliwa hapa hapa nchini.

“Na tukifanya hivyo tayari tutakuwa tumefanikiwa kuitangaza nchi yetu vizuri kwani tutakuwa tunauza korosho ambazo zimebanguliwa hapa hapa nchini”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...