Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Awamu ya Sita Dkt. George Mark Fihavango akiipongeza Serikali kwa kuleta maendeleo nchini mara baada ya kusimikwa kuwa askofu wa Dayosisi hiyo katika Ibada takatifu iliyofanyika Mjini Njombe na kuongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Frederick Shoo (hayupo pichani).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika ibada ya kumsimika Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Awamu ya Sita Dkt. George Mark Fihavango iliyofanyika Mjini Njombe na kuongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Frederick Shoo (hayupo pichani)
Baadhi ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na madhehebu mengine wakishiriki ibada ya kumsimika Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Awamu ya Sita Dkt. George Mark Fihavango iliyofanyika Mjini Njombe na kuongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Frederick Shoo (hayupo pichani)
Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Frederick Shoo akimpongeza Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake kwa kuwaletea watanzania maendeleo, pongezi hizo amezitoa mbele ya waumini wa KKKT na madhehebu mengine wakati wa ibada ya kumsimika Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Awamu ya Sita Dkt. George Mark Fihavango iliyofanyika mjini Njombe.

……………………..

Na James K. Mwanamyoto – Njombe

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeipongeza Serikali kwa kuleta maendeleo katika miundombinu ya barabara, reli na anga, kuhimiza maendeleo ya viwanda ili kuwawezesha watanzania kuuza bidhaa zilizoandaliwa, ikiwa ni pamoja na kutoa uhuru wa kila mtanzania kuabudu. 

Pongezi hizo zimetolewa na Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Awamu ya Sita Dkt. George Mark Fihavango mara baada ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Dayosisi hiyo katika Ibada Takatifu iliyofanyika jana Mjini Njombe na kuongozwa na Mkuu wa KKKT, Baba Askofu Dkt. Frederick Shoo.

Askofu Fihavango amesema, Kanisa linaishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Dayosisi yake hususani katika sekta ya afya.

Dayosisi yangu ina ubia na Serikali wa kutoa huduma za afya kupitia Hospitali Teule ya Kilutheri Ilembula iliyopo Wangingombe ambapo kati ya watumishi 182 waliopo, Serikali inalipa mishahara watumishi 110 kupitia mfuko wa ruzuku, amefafanua Dkt. Fihavango.

Askofu Fihavango ameongeza kuwa, Serikali imekuwa ikitoa fedha na vifaa tiba kwenye hospitali hiyo ili kuwezesha utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wananchi, akitoa mfano katika mwaka wa fedha 2018/19 hospitali imepokea jumla ya shilingi 187,421,791/= na ruzuku ya mishahara ya watumishi kiasi cha shilingi 1,056,168,000/=.

Kama haitoshi, Askofu Fihavango ameeleza kuwa, Serikali imetoa gari la wagonjwa kwa Hospitali ya Kilutheri Ilembula na Kituo cha Afya Kidugala ambalo limesaidia kuboresha huduma za afya hasa za mama na mtoto hivyo inaonyesha dhahiri kuwa kanisa na Serikali ni washirika katika kuleta maendeleo ya taifa.

Akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika ibada hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) ametoa pongezi kwa KKKT kwa kushirikiana na Serikali kuwaletea maendeleo wananchi.

Mhe. Mkuchika amesema, Serikali inatambua mchango wa kanisa hilo katika kutoa huduma za kiroho, afya, elimu na uchumi bila kubagua wananchi kwa kigezo cha utofauti wa dini, hivyo limekuwa na mchango katika maendeleo ya taifa na kulitaka kuwahimiza waumini wake kutokwepa kulipa kodi ili Serikali ipate fedha za kuendesha shughuli za maendeleo.

“Katika kutoa huduma za afya, Serikali inaendelea kushirikiana na kanisa kutoa huduma hiyo kupitia Hospitali Teule ya Ilembula na Kituo cha Afya Kidugalo na zahanati nyinginezo ambazo ni mali ya KKKT Dayosisi ya Kusini” Mhe. Mkuchika ameongeza.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa Serikali inatoa vifaa tiba na mishahara kwa watumishi wa Hospitali Teule ya Ilembula ambao 110 ni wa kanisa na 37 wa Serikali ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za matibabu.

Aidha, Mhe. Mkuchika ametoa wito kwa KKKT kuendelea kushirikiana na Serikali katika kushauriana na kudumisha utamaduni wa kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu ustawi na maendeleo ya wananchi kwa lengo la kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Kwa upande wake, Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Frederick Shoo amempongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake kwa kuwaletea watanzania maendeleo katika sekta ya afya, elimu na nishati.

Askofu Dkt. Shoo, pia hakusita kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kurejesha nidhamu ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kwani nidhamu ya watumishi wa umma imekuwa ni chachu ya maendeleo katika taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Ibada ya kumsimika Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini, Dkt. George Mark Fihavango iliyofanyika Njombe, Oktoba 13, 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...