MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imekubali maombi ya Chama cha ACT- Wazalendo kujiunga katika kesi ya kikatiba inayohusu ukomo wa urais, iliyofunguliwa na mwananchi anayejitambulisha kama mkulima, Dezydelius Patrick Mgoya.

 Uamuzi huo umetolewa leo Alhamis, Oktoba 24, 2029 na Jaji Dk. Benhajj Masoud , baada ya kuridhika na hoja za chama hicho kuwa kina maslahi katika shauri hilo.

Kesi hiyo ya Mgoya imefungua mahakamani hapo, masjala Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiiomba mahakama itoe tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya Ibara ya 40(2) ya Katiba ya Nchi inayoweka ukomo wa mtu kuchaguliwa kuwa rais.

Katika Maombi hayo, Mgoya anadai kuwa masharti ya ibara hiyo ya 40(2) ya mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais yaani miaka 10 tu yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) hasa kushiriki katika shughuli za utawala kwa kuchagua na kuchaguliwa.

Hata hivyo Serikali kupitia kwa AG tayari imeshamwekea pingamizi la awali ikiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali pamoja na mambo mengine ikidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, na kwamba kesi hiyo ina kasoro za kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.

Pia inadai kuwa mwombaji hana haki ya kisheria kufungua na kwamba nafuu anazoziomba mwombaji haziwezi kutolewa kwa kuwa zinakiuka kifungu cha 44 cha Sheria ya Mawakili, Sura ya 341, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hata hivyo, kabla ya mahakama hiyo kusikiliza pingamizi hilo la Serikali Bodi ya Wadhamini wa ACT, iliwasilisha mahakamani hapo maombi ya kujiunga katika kesi hiyo, kama mdaawa mwenye maslahi, kwa madai kuwa wana maslahi nayo na kwamba wanataka kutetea kile wanachokiita maslahi yao.

 Muombaji Mgoya kwa upande wake alipinga maombi hayo, pamoja na mambo mengine akidai kuwa chama hicho hakina sababu za msingi za kuunganishwa katika kesi hiyo hoja ambazo zinetupiliwa mbali na mahakama kuu ikisema kuwa chama hicho kina haki ya kuunganishwa.

Jaji Masoud amesema kuwa katika mashauri ya kikatiba mtu yeyote awe na maslahi binafsi au asiwe na maslahi binafsi anaweza kuwasilisha maombi mahakamani na kwamba kwa kuwa shauri lililoko mahakamani ni la kikatiba basi mwombaji (ACT_Wazalendo) kina maslahi katika shauri hilo.

Katika shauri la msingi linalosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Kiongozi, Dk. Elieza Feleshi, akishirikiana na Jaji Dk. Masoud na Jaji Seif Kulita, limepangwa kutajwa mahakamani hapo kesho kwa ajili ya mahakama kutoa maelekezo maalum.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...