Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
BARAZA la Habari Tanzania (MCT) limetangaza kuanza mchakato wa kutoa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari (Ejat)  kwa waandishi waliofanya vizuri katika makundi mbalimbali 2019 na kuongeza makundi mapya ikiwemo uandishi wa habari za ubunifu na maendeleo ya watu ambazo zitatolewa na HDIF

Pazia hilo limefunguliwa leo Oktoba 11,2019 na kutoa fursa kwa wanahabari kuwasilisha kazi zao zenye kuzingatia viwango na misingi ya uandishi ili kushiriki kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT 2019, Kajubi Mukajanga amesema tuzo za mwaka huu zitakuwa ni za 11 Kufanyika ambapo ambapo kwa mara ya kwanza zilifanyika 2009.

Ameyataja makundi mengine mapya ni tuzo ya uandishi wa hedhi salama na habari za afya ya uzazi huku makundi ya habari za usalama na ubora wa chakula, habari za kodi na mapato na habari za afya hazitakuwepo.

Amesema washirika wa tuzo hizo za  EJAT ni pamoja na taasisi za Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-TAN), wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA),  Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Hakielimu, Sikika, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT).

Aidha tuzo zitakazotolewa ni zile za uandishi wa habari za uchumi na biashara na fedha, uandishi wa habari za michezo na utamaduni, uandishi wa habari za biashara na kilimo, uandishi wa habari za elimu, uandishi wa habari za utalii na uhifadhi na uandishi wa habari za uchunguzi.

"Makundi mengine ni uandishi wa takwimu, uandishi habari za haki za binadamu na utawala bora, mpigapicha bora magazeti, mpigapicha bora redio, mchorakatuni bora, uandishi wa habari za jinsia, uandishi wa habari za wazee, watoto, habari za gesi, mafuta na uchimbaji madini, habari za afya ya uzazi, habari za ubunifu na maendeleo ya watu, habari za usalama barabarani, hedhi usalama na kundi la wazi," alifafanua Mukajanga.

Mukajanga amesema, MCT hutoa udhamini wa Sh milioni 3, kwa mshindi wa jumla ili ajiendeleze kitaaluma katika masuala ya uandishi wa habari kulingana na mahitaji yake.

Mukajanga alisema waandishi wa habari wanapaswa kuwasilisha kazi zao kuanzia Oktoba 11,2019  hadi Januari 31, 2020.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Ubunifu (HDIF), Hannah Mwandoloma amesema wameingia kudhamini tuzo za uandishi wa habari za ubunifu na maendeleo ya watu kwa lengo la kuwavumbua wabunifu waliopo katika jamii ili waweze kujulikana.

"Tunahamasisha waandishi wa habari kuandika habari za ubunifu zitakazochochea mabadiliko chanya na kuwasaidia wabunifu wadogo wapate mitaji kwani uandishi wa habari za ubunifu utawasaidia wabunifu wenyewe kutambua sera zilizopo katika kufikia malengo yao" Amesema.

Amesema, HDIF imetoa fedha kwa mashirika 40 ambayo yanafanya kazi katika sekta za elimu, afya na maji hivyo, katika kudhamini tuzo hizi wanaimani wabunifu wengi watagundulika ameongeza kusema kuwa wataendelea kusapoti tuzo na kuwathamini waandishi wa habari.

Naye, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wadau wa Hedhi Salama, Wilhelmina Malima amesema waandishi wa tuzo hizo, watasaidia kuvunja ukimya uliopo katika jamii na kuongeza upatikanaji wa taarifa za hedhi salama pia zitasaidia kuvumbua masuala mbalimbali kuhusu upatikanaji wa vifaa na miundombinu rafiki kwa wasichana na wanawake pamoja na upatikanaji wa bidhaa kwa gharama nafuu.
 Katibu wa Baraza la Habari nchini (MCT), Kajubi Mukajanga (katikati), Mtaalamu wa mawasiliano kutoka Mfuko wa maendeleo ya jamii na ubunifu endelevu (HDIF), Hannah Mwandoloma (kushoto) na Meneja program wa baraza hilo, David Mbulumi wakionyesha fomu za ushiriki wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari (Ejat), wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo uliofanyika jijini Dar es Salaam
Katibu wa Baraza la Habari nchini (MCT), Kajubi Mukajanga (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa tuzo za umahiri za uandishi wa habari (Ejat), uliofanyika leo katika ofisi za MCT jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni mtaalamu wa mawasiliano kutoka Mfuko wa maendeleo ya jamii na ubunifu endelevu (HDIF), Hannah Mwandoloma (kushoto) na Meneja program wa baraza hilo, David Mbulumi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...