Muonekano wa mradi wa Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, Jijini Dodoma unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Kamishna Msaidizi wa masuala ya Nishati ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga akitoa maelezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya AfDB, Bw. Amos Cheptoo (kushoto), katika chumba cha mitambo ya kupozea umeme katika mradi wa Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, Jijini Dodoma.
Mratibu wa mradi wa Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, Jijini Dodoma, Mhandisi Peter Kigandye (wa kwanza kushoto), akieleza utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Umeme cha Zuzu ambapo unatarajia kukamilika Februari, 2020, wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bw. Amos Cheptoo (kushoto) ya kukagua mradi huo Jijini Dodoma.(Picha na Peter Haule, WFM, Dodoma)


Na Peter Haule, WFN, Dodoma

Benki ya Maendeleo ya Afrika – AfDB imeridhishwa na kasi ya maendeleo ya mradi wa Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu kinachofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan- JICA.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya AfDB, Bw. Amos Cheptoo, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Kituo hicho kilichopo katika eneo la Zuzu Mkoani Dodoma.

Bw. Cheptoo alisema kuwa amejionea kazi nzuri inayofanywa na Mkandarasi ya kuhakikisha mradi huo unakamilika Februari, 2020 na kutumika kikamilifu katika kupoza na kusambaza umeme kwa manufaa ya Tanzania na nchi jirani.

Alisema kuwa mradi huo utakua na tija zaidi baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere unaotarajia kuzalisha zaidi ya Megawati 2000, hivyo kuifanya miundombinu ya kupoza umeme kutumika kimailifu.

Mkurugenzi huyo wa AfDB alisema umeme ndio nyenzo muhimu katika ukuzaji wa uchumi na uendelezaji wa viwanda katika nchi za Afrika, kukamilika kwa miradi ya umeme kutasaidia uwepo wa umeme wa kutosha hasa katika nchi za Afrika mashariki na kusini mwa Afrika.

Serikali ya Tanzania imechukua hatua nzuri za kuboresha miundombinu wezeshi ya uzalishaji hasa Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya nchi.

Kwa upande wake mratibu wa mradi huo Mhandisi Peter Kigandye alisema kuwa, mradi huo utakuwa na uwezo wa kushusha umeme kwa Kilovoti 400 na kupoza umeme wenye uwezo wa takribani megawati 400 kisha kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.

Gharama ya mradi huo unajumuisha mradi mwingine uliopo Singida na gharama zake ni dola za Marekani milioni 53 ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Benki ya AfDB na Shirika la JICA ambapo Kituo cha Kupozea Umeme cha Zuzu kinagharimu takribani dola za Marekani milioni 22.

Aidha Kamishna Msaidizi wa masuala ya Nishati ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga, ameishukuru Benki ya AfDB kwa kusaidia uboreshaji wa miundombinu hasa ya umeme kwa kuwa miradi hiyo itakapokamilika, utazinufaisha pia nchi za Zambia, Botswana na hata Afrika ya Kusini, kupitia mtandao wa umeme wa kusini

Amewataka wawekezaji walio na nia ya kuwekeza Dodoma kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuwekeza hasa katika viwanda vikubwa na vidogo kwa kuwa mazingira ya uwekezaji yapo vizuri.

Mhandisi Luoga ameiomba Benki ya AfDB kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya usambazaji zaidi wa umeme katika Mkoa wa Dodoma na viunga vyake ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kulifanya jiji kuwa na hadhi stahiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...