TAASISI ya Wakfu ya Citi kwa kushirikiana na Shirikisho la Asasi zinazotoa huduma za fedha kwa wajasiriamali wadogo (TAMFI), imezindua shindano la kuwania tuzo ya wakfu huo kwa wajasirimali wadogo jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zimelenga kuangalia mchango usio wa kawaida kwa wajasiriamali wadogo katika kuimarisha uchumi wao binafsi katika ngazi ya familia na kijamii nchini kote.

Akizindua shindano hilo mwishoni mwa wiki, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Citibank Tanzania, Geofrey Mchangila, alisema tuzo hizo ambazo zimeota mizizi nchini katika miaka mitatu iliyopita, zimeonesha mafanikio kwa baadhi ya wajasiriamali waliokuwa wabunifu.

“Zaidi ya shilingi milioni 70 zitatuzwa kwa washindi 16 na fedha hizo zitakwenda sanjari na kuhimiza mchango wa taasisi ndogo za kifedha (MFIs) na wajasirimali wadogo nchini Tanzania ” alisema.

Kuanzia mwaka 2005, tuzo za wajasiriamali wadogo, zimejikita zaidi katika kuamsha fursa za kukua kwa ujasiriamali mdogo katika nchi takribani 30.

Kwa mujibu wa Mchangila, tuzo hizo zinaboresha ujumuishaji wa fedha na kuzalisha utambulisho kwa wajasiriamali, waliofanya ya ziada katika kuhakikisha kwamba wanajiwezesha kiuchumi wao na familia zao na kuchangia uchumi wa jamii zao na uchumi wa taifa.

Mtendaji mkuu wa TAMFI, Winnie Terry, alisema tuzo hizo ni chachu katika kuonesha jamii kwamba ukopaji wa fedha na ulipaji wenye nidhamu unalipa na kwamba ni ufunguo katika maendeleo ya kiuchumi.

Terry aliongeza: “Katika miaka miaka mitatu iliyopita, zaidi ya wajasiriamali 45 walioteuliwa katika taasisi zao zilizowakopesha fedha za mtaji walijipatia zaidi ya Sh milioni 210 katika tuzo hizo.”

Tuzo hizo zitashindaniwa katika ngazi mbalimbali kwa kuzingatia jinsia, uchumi na idadi ya rasilimali watu. Aidha, biashara hiyo iwe na athari chanya kwa mjasiriamali, familia yake na jamii kwa ujumla.

Washiriki katika tuzo hizo nchini, watawasilisha kazi zao kwa majaji ambao ni wabobezi katika masuala ya fedha, viongozi wa taasisi binafsi na umma na wanazuoni katika sekta ya ujasiriamali.

Mchakato wa kumpata mshindi katika tuzo hizo, utafanyika Juni 2020 na washindi kutangazwa baadaye katika hafla itakayofanyika jijini Dar es salaam.

Mpaka sasa Wakfu wa Citi umewekeza jumla ya Dola za Marekani milioni 23.5 katika mitandao ya taasisi ndogo za kifedha na kutoa tuzo za Dola za Marekani milioni 10.5 kwa zaidi ya wajasiriamali 6,000.
Ofisa Mtendaji mkuu wa Citibank Tanzania , Geofrey Mchangila (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kueleza uzinduzi wa awamu ya nne ya tuzo za wajasiriamali wadogo zinazoendeshwa na Wakfu wa CITI , Dar es salaam Tanzania mwishoni mwa. Kulia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Asasi zinazotoa huduma za fedha kwa wajasiriamali wadogo (TAMFI) Joel Mwakitalu, na Makamu Rais wa Citi, Dorbibi Jemadari
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...