Veronica Simba – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Nishati, inakamilisha mradi mkubwa wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme kilichopo Zuzu Dodoma, ambacho baada ya kukamilika kitakuwa na uwezo wa megawati zaidi ya 600, hivyo kuongoza Tanzania nzima kwa wingi wa umeme.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, Februari 19, 2020 alipofanya ziara katika kituo hicho kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi husika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri amebainisha kuwa, kwa kiasi hicho cha umeme (megawati 640), Dodoma italipita hata jiji la Dar es Salaam ambalo linaongoza kwa sasa kwa kuwa na megawati takribani 587.

“Napenda niishukuru sana Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Rais kwa kutupatia Dola za Marekani milioni 52 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu,” amesema.
Akifafanua zaidi kuhusu manufaa ya mradi huo, Dkt Kalemani amesema mbali na kutosheleza mahitaji ya kawaida ya wananchi, kiasi hicho cha umeme pia kitawezesha uwekezaji wa viwanda vya aina mbalimbali hivyo kukuza uchumi.

Ameeleza zaidi kuwa, dhamira ya serikali kutekeleza mradi huo ni kutokana na ongezeko la mahitaji ya umeme mkoani humu ambayo yamepanda kutoka wastani wa megawati 15 hadi kufikia megawati 40 kwa siku.

Amesema, ongezeko hilo la mahitaji linaweza kusababisha uhaba wa nishati ya umeme Dodoma endapo hazitachukuliwa hatua za makusudi na haraka katika kulitafutia ufumbuzi na kuongeza kuwa, ndiyo maana serikali imeagiza mradi huo ukamilike na kukabidhiwa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari, 2020.

“Kasi ya kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi Dodoma ni kubwa. Tukizembea, hali inaweza kuwa mbaya, jambo ambalo serikali haiwezi kuruhusu litokee.
Kufuatia umuhimu wa kukamilika kwa mradi huo mapema, Waziri amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya KCE kutoka India, kufanya kazi usiku na mchana ili akamilishe kazi kwa wakati huku akisisitiza kuwa kamwe hataongezewa muda.

Katika hatua nyingine, Waziri ameuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupitia kwa Msimamizi wa Mradi husika, Mhandisi Peter Kigadye, kushughulikia malalamiko ya wananchi wanaoishi jirani na Kituo hicho ambayo ni pamoja na kuunganishiwa huduma ya umeme pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.

Hii ni mara ya tatu kwa Waziri Kalemani kufanya ziara katika kituo hicho ili kujionea maendeleo ya mradi husika tangu ulipoanzwa kutekelezwa Machi, 2018.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto), akitoa maelekezo kwa mkandarasi (Kampuni ya KCE) anayetekeleza mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Zuzu, Dodoma, alipofanya ziara kukagua maendeleo ya mradi huo, Februari 19, 2020.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akitoa maelekezo kwa mkandarasi (Kampuni ya KCE) anayetekeleza mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Zuzu, Dodoma, alipofanya ziara kukagua maendeleo ya mradi huo, Februari 19, 2020.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akitoa maelekezo kwa mkandarasi (Kampuni ya KCE) anayetekeleza mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Zuzu, Dodoma, alipofanya ziara kukagua maendeleo ya mradi huo, Februari 19, 2020.
 Taswira mbalimbali zikionesha hatua iliyofikiwa katika kutekeleza mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Zuzu, Dodoma. Taswira hizi zilinaswa Februari 19, 2020 wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani).
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Zuzu, Dodoma Februari 19, 2020.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akizungumza na wananchi wanaoishi jirani na kituo cha kupoza umeme Zuzu Dodoma, alipokuwa katika ziara kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa kituo hicho, Februari 19, 2020.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...