Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ( wa pili kushoto) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye eneo la Sinai Wilayani Mufindi kwenye ziara yake aliyoifanya Mkoani Iringa tarehe 15 Februari, 2020 yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini. Kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Abdulrahman Milandu.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika machimbo ya dhahabu ya Sinai yaliyopo Wilayani Mufindi Mkoani Iringa akitoa maoni yake kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (hayupo pichani) kwenye mkutano na wachimbaji hao ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa wa Iringa aliyoifanya tarehe 15 Februari, 2020 yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

******************************
Na Greyson Mwase, Iringa

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa nchini kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili Tume ya Madini iweze kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019/2020 la shilingi bilioni 470.

Profesa Kikula alitoa kauli yake jana tarehe 15 Februari, 2020 mkoani Iringa kwenye ziara yake ya kikazi katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kuzungumza na wachimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Katika ziara yake Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Abdulrahman Milandu, pamoja na timu ya wataalam kutoka Ofisi ya AfisaMadini Mkazi wa Mkoa wa Iringa na kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini.

Alisema kuwa, mchango wa Sekta ya Madini unategemewa sana kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo wataalam kwenye Sekta hawana budi kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanakusanya maduhuli huku wakidhibiti utoroshwaji wa madini.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini, Profesa Kikula alifafanua kuwa ni pamoja na kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ambapokatika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilikusanya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 346 ikiwa imevuka lengo lililopangwa la kukusanya shilingi bilioni 310.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa pamoja na Maafisa Migodi Wakazi kwenye maeneo yenye migodimikubwa ya madini, uanzishwaji wa masoko ya madini pamoja na vituo vya ununuzi wa madini.

Aliendelea kusema kuwa ili kuhakikisha huduma katika shughuli za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini zinaimarika nchini, Serikali imeongeza wataalam kwenye Ofisi za Madini, vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari na mashine za kupima madini kwenye masoko ya madini yaliyoanzishwa.

Aidha, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanaandaa na kutekeleza mipango ya ufungaji wa migodi ili kuepusha athari za uharibifu wamazingira zinazoweza kujitokeza mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini.

Vilevile aliwataka wachimbaji wa madini kuendesha shughuli zao kwa kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

Profesa Kikula alitembelea machimbo ya mchanga yaliyopo katika Kambi ya Jeshi la Magereza la Mlolo yaliyopo Wilayani Iringa, Machimbo ya mchanga ya Ifingo Wilayani Mufindi na Machimbo ya Dhahabu ya Sinai, Ugenza Wilayani Mufindi, mkoani Iringa.

Akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Sinai Wilayani Mufindi Mkoani Iringa, Profesa Kikula aliwataka wachimbaji hao kutumiamasoko ya madini yaliyoanzishwa na kuongeza kuwa upo utaratibu wa kusogeza huduma kwa kuweka vituo vya ununuzi wa madini ili waweze kunufaika.

Aidha aliwataka wachimbaji hao kujiepusha na migogoro na kuwahakikishia kuwa Serikali ipo tayari kuwasaidia katika kuhakikisha kuwa uchimbaji wao na unakuwa na faida.

Aidha, Profesa Kikula alimpongeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa kwa utekelezaji wa mikakati aliyojiwekea kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini katika Mkoa wa Iringa.

Wakati huohuo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Abdulrahman Milandu akielezea namna wanavyosimamia shughuli za madini katika mkoa huo, alisema kuwa wachimbaji wengi hususan wa madini ya ujenzi wameanza kuchimba kulingana na Sheria ya Madini na Kanuni zake inavyotaka kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na ofisi yake.

Alisema tayari ofisi yake imetoa elimu kwa wachimbaji wa madini na wananchi kuhusu mpango wa utoaji wa huduma kwa jamii katika migodi ya dhahabu ya Nyakavangala, Ihanzutwa, Ulata, Uengulinyi, Lupembe Senga na katika maeneo ya uchimbaji wa mchanga, udongo na mawe katika vijiji vya Kibena, Muwimbi, Rungemba, Kikiombo,Saohill, Isakalilo na Kitelewasi vilivyopo katika Wilaya za Iringa na Mufindi.

Aliongeza kuwa Ofisi yake imeanza kuhamasisha wachimbaji wa madini ujenzi na watengenezaji wa tofali kuunda vikundi vidogo na kupewa leseni za madini.

“Tunaamini kuwepo kwa vikundi rasmi vya wachimbaji wa madini ujenzi na watengenezaji wa tofali kutachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuliya Serikali”. Alisema Mhandisi Milandu.

Katika hatua nyingine Mhandisi Milandu alisema katika kuhakikisha hakuna utoroshaji wa madini ujenzi katika mkoa wa Iringa, Ofisi yake imekuwa ikishirikiana kwa karibu zaidi na vyombo vya ulinzi na usalama kama vile jeshi la polisi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...