Na Karama Kenyunko, Michuzi Globu ya jamii.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika  kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Ofisa Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Tito Magoti (26) na mwenzake kueleza hali ya upelelezi umefikia wapi kama unakwenda mbele au la.

Tito anashtakiwa na mwenzake mbaye ni mtaalamu wa masuala ya Tehama Theodory Gyan (36) ambapo wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha wa Sh.milioni 17, 354,535
Amri hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega baada upande wa mashtaka kudai kesi hiyo leo Februari 19, mwaka 2020 imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi bado haujakamilika.

Kutokana na taarifa hiyo, jopo la mawakili saba wa utetezi, wakiongozwa na Fulgence Massawe akisaidiana na Anna Henga pamoja na Jembra Kambole walidai Februari 2, mwaka huu upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua nzuri kwani wanachunguza masuala ya teknolojia na unahusisha nchi mbalimbali.

"Leo ni mara ya tano kesi hii inatajwa na kila usiku wanaambiwa upelelezi uko kwenye hatua nzuri sasa tunaona kama tunarudi nyuma hivyo tunaomba mahakama iamuru upelelezi ukamilike na upande wa mashitaka wasiende mbele na kurudi nyuma," amedai Henga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Wakili Jebra Kambole ameiomba Mahakama kutumia mamlaka iliyonayo kuudhibiti upande wa mashtaka kuhusu upelelezi wa kesi hiyo kwa madai kwamba hakuna mtu anayejua upelelezi huo utakamilika lini hivyo, sio tabia njema kwa upande wa mashitaka kubadilisha maneno kuhusu upelelezi huo.

Aliendelea kudai Mahakama hiyo inatambua kuwa washitakiwa wako rumande na hawana dhamana na kwamba wanafamilia ambazo zinahitaji misaada yao hivyo wanaomba upande wa serikali waeleze hatua zilizofikiwa kwenye upelelezi uliopita ili mahakama na washtakiwa wajue.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedPai watahimiza wapelelezi kukamilisha maeneo yaliyosalia ili yakamilishwe haraka iwezekanavyo.

Alidai ni hatari katika hatua hiyo ya upelelezi kuingia ndani kuelezea yanayofanywa na wapelelezi wakati shauri bado halijaanza kusikilizwa.
"Wadau wana haki ya kusikiliza kesi hiyo na niwatoe wasiwasi kwamba wawekezaji wanaipenda Tanzania na watakuja kuwekeza. Lakini pia mahakama bado haijapokea taarifa kuhusu hatua ya uandaaji wa maelezo ya washitakiwa," alidai Simon.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mtega amesema upande wa mashitaka uhakikishe unakidhi amri iliyotolewa Februari 5, mwaka huu na wakija tena waeleze hatua halisi ya upelelezi ulipofikia hatua gani ili mahakama ijue upelelezi unakwenda mbele au la na sio kueleza kwa ujumla.

Washitakiwa hao wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania kwa pamoja na watu ambao hawapo mahakamani kwa makusudi walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya Kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia kiasi cha Sh.17,354,535.

Katika  mashitaka ya pili, inadaiwa  katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji na Mkoa wa Dar es Salaam kwa pamoja washitakiwa hao na mengine ambao hawapo mahakamani walimiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kutenda makosa ya jinai.

Pia inadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, mwaka huu, ndani ya jiji la Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walijipatia jumla ya Sh 17,353,535 wakati wakijua mapato hayo yametokana na mazalia ya kosa la kushiriki genge la uhalifu.

Washitakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwakuwa mahakama hiyo aina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi mpaka ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mshitaka nchini (DPP).
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...