Charles James, Michuzi TV

TANZANIA imepiga hatua kubwa katika kutoa nafasi kwa wanawake kwenye nafasi za uongozi kulinganisha na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wakati akizindua mtandao wa wanawake viongozi kwa bara la Afrika tawi la Tanzania (AWLN).

Amesema licha ya Nchi za kiafrika kutoa nafasi ndogo kwa wanawake kwenye ngazi za kimaamuzi lakini serikali nchini imepiga hatua wa kuvuka kiwango cha juu cha angalau asilimia 30 kilichowekwa na Nchi wanachama wa SADC.

Mama Samia amesema mathalani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye jumla ya wabunge 393 idadi ya wabunge wanawake ni 126 sawa na asilimia 36 huku Baraza la wawakilishi Zanzibar likiwa na asilimia 38 ya wawakilishi wanawake kwenye Baraza lake.

Kwa upande wa Mahakama Majaji wanawake kwa Mahakama Kuu ni asilimia 30 wakati Mahakama ya Rufaa Majaji wanawake wakiwa asilimia 38 huku Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiwa na asilimia 18 ya Mawaziri wanawake na asilimia 33 ya Naibu Mawaziri wanawake.

" Pamoja na kutopiga hatua sana kwenye kuwapa wanawake nafasi za uongozi lakini angalau Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kufikia usawa wa kijinsia kwani ukiachana na takwimu hizo hapo bado wanawake wamewahi kupata nafasi za kugombea hadi nafasi ya Urais.

Pia tumewahi kuwa na Spika Mwanamke katika Bunge lililopita, Mama Anne Makinda na bunge la sasa tunae Naibu Spika Dk Tulia Ackson na zaidi tuna Makamu wa Rais mwanamke, hiyo yote ni kuonesha jinsi gani tunazidi kupiga hatua," Amesema Mama Samia.

Amesema kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu, Wanawake nchini wanatakiwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kupata fursa ya kuwepo kwenye nafasi za maamuzi.

Mama Samia amewataka wanawake nchini kujitokeza kugombea nafasi zilizopo na kwa wingi walionao wanawake nchini kama wakipeana ushirikiano unaotakiwa ni rahisi kufikia asilimia 50/50 kwenye nafasi za uongozi nchini.

Amesema kuna faida kubwa kwa wanawake kuwa viongozi kwani kumesaidia ongezeko la bajeti pamoja na maendeleo kwenye sekta nyingi ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

" Ngojeni niwanong'onezeni, mwaka huu ni wa uchaguzi na sasa vyama vyote vya kisiasa vipo kwenye mchakato wa kuandika ilani zao, jipenyezeni huko mpigie kelele asilimia 50/50 kwenye nafasi za uongozi.

Tumeshuhudia namna ambavyo taasisi na mashirika yanayoongozwa na wanawake yanavyopiga hatua kwa sababu ya uaminifu, ustadi na weledi ambao wakina mama tumekua nao pindi tunavyopewa nafasi ya kuongoza," Amesema Mama Samia.

Amepongeza Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wanawake (UN Women) kwa kuratibu uanzishwaji wa mtandao huo ambao amesema kama utatumika vizuri utasaidia kukuza idadi ya wanawake viongozi barani Afrika na Tanzania kwa ujumla.

Akizungumza awali Mwenyekiti wa Kamisheni Maalum ya Wanawake, Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika, Bi Bineta Diop amesema anaamini mtandao huo utakwenda kukuza na kuongeza zaidi wingi wa viongozi wanawake walio bora.

Bi Diop amesema kwa muda mrefu Tanzania imekua ni kitovu cha viongozi wanawake na uwepo wa Makamu wa Rais mwanamke ni kielelezo tosha cha namna gani kama Taifa kumekua na utaratibu wa kutoa nafasi za kimaamuzi kwa wanawake kulinganisha na Nchi nyingine za Kiafrika.

Kwa upande wake mmoja wa wanachama wa Mtandao huo, Dk Gertrude Mongella amemshukuru Mama Samia kwa kuwafungulia mtandao huo kwani anaamini mtandao huo utakua daraja la wanawake viongozi vijana kufikia malengo yao.

" Huu siyo mtandao wa watu Fulani, ni mtandao wa kila mtu kuanzia wanawake wa mjini hadi kijijini tunahitaji kufikia malengo yetu kwa kuhakikisha tunapigania usawa bila kuchoka.

Tunaamini uwepo wa Mama Samia hapa ni kielelezo tosha cha kwamba serikali iko pamoja na sisi na sisi tuna wajibu pia wa kushirikiana na serikali katika kutokomeza mila potofu zilizopo nchini juu ya wanawake," Amesema Mama Samia.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Spika Dk Tulia Ackson, Mabalozi wa Nchi mbalimbali, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge na wanawake viongozi kutoka taasisi na mashirika tofauti ambapo wameshuhudia Tanzania ikiwa Nchi ya 14 kuzindua mtandao wa wanawake viongozi Afrika kwa ngazi ya Kitaifa.
 Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu akikabidhiwa zawadi ya kanga kutoka kwa Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Wanawake nchini, Hodan Addou wakati wa uzinduzi wa mtandao wa wanawake viongozi Afrika tawi la Tanzania.
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtandao wa wanawake viongozi Afrika tawi la Tanzania. Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
 Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wabunge wanawake waliojitokeza kwenye uzinduzi wa mtandao wa wanawake viongozi Afrika tawi la Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...