Charles James, Michuzi TV

MTANDAO wa Viongozi Wanawake wa Afrika (AWLN) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Wanawake UN Women kesho wanatarajia kuzindua tawi lao nchini ambapo mgeni rasmi atakua Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan.

Uzinduzi huo utafanyika jijini Dodoma ambapo utahusisha viongozi 60 wanawake pamoja na wageni walioalikwa wakiwemo watendaji kutoka serikalini, Umoja wa Mataifa, Wajumbe wa kibalozi na Umoja wa Afrika.

Akizungumza leo na wandishi wa habari, Mwenyekiti Mwenza wa Mtandao huo, Mary Rusimbi amesema mtandao huo umekusudia kuboresha uongozi wa wanawake katika kuleta mabadiliko barani Afrika, sanjari na ajenda ya Afrika 2063 na malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030.

Amesema lengo la sita yaani la ajenda ya Afrika 2063, "Afrika Tunayoitaka" inadhamiria kuona Afrika iliyojikita katika maslahi ya watu, inayojumuisha usawa wa kijinsia na ambapo wanawake wanawezeshwa kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za maisha.

" Ni jambo linalotambulika sana kwamba licha ya maendeleo yaliyofanywa kote barani Afrika kuhusu swala la usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, mambo mengi bado yanapaswa kufanyika ili wanawake wapate haki zao kikamilifu na usawa na kuruhusu ushiriki wao katika vuguvugu la mabadiliko.

Mtandao wetu unajitahidi kutumika kama jukwaa la kuhamasisha wanawake katika sekta mbalimbali ili kushadidisha kikamilifu hatua zinazoelekea kuleta amani na maendeleo na kutumika kama zana jumuishi ya kuzuia migogoro kwa kuhakikisha ushiriki wa wanawake," Amesema Rusimbi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa UN Women nchini, Hodan Addou amesema mtandao huo haulengi kuwahamasisha wanawake katika uongozi wa kisiasa pekee bali uongozi ambao utaanzia katika ngazi ya awali kwenye jamii zao.

" Watu wengi hufikiria nafasi za uongozi za kisiasa kwa maana ya Wabunge, Wakuu wa Wilaya au Wakurugenzi lakini mwanamke anaweza kuanzia katika nafasi za chini kabisa kwenye jamii. Nitoe rai kwa wanawake kupenda kujitokeza kuchukua nasi kwenye nafasi zote za uongozi," Amesema Hodan.

Mmoja wa wawezeshaji kwenye mkutano huo, Gertrude Mongella amesema mtandao huo utawezesha uhusiano thabiti miongoni mwa wanawake katika ngazi za kijamii, kitaifa na kikanda na itahusisha wanawake kutoka katika makundi ya kijamii.

" Ni lazima kama wanawake tupambane kuonesha heshima yetu na nguvu tuliyonayo kwenye jamii, mtandao wetu ukawe kimbilio lakini mwanamke kwenye maeneo yetu.

Hatupo hapa kuchukua nafasi za watu wengine lakini tunahitaji kukua na kuhakikisha kwamba hata Serikali ikiwa inafikiria kutunga sera za wanawake basi ifikirie kuanza na mtandao wa Viongozi Wanawake," Amesema Dk Mongella.

Hadi sasa Nchi 11 zimefanikiwa kuzindua ofisi zao za kitaifa ni pamoja na DR Congo, Ivory Coast, Nigeria, Jamhuri ya Afrika Kati, Sierra Leone, Kongo Brazzaville, Shelisheli, Morocco, Cameroon, Liberia, Ethiopia na sasa Tanzania.
Mwakilishi wa Shirika La Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Wanawake UN Women, Hodan Addou akizungumzia ushirikiano wao kwa mtandao huo wa wanawake viongozi was Afrika tawi la Tanzania.

 Mwenyekiti Mwenza wa Mtandao wa Viongozi Wanawake wa Afrika tawi la Tanzania, Mary Rusimbi akielezea dhima ya uanzishwaji wa mtandao huo katika mkutano na wandishi wa habari leo jijini Dodoma.
 Mwezeshaji wa mkutano wa mtandao wa wanawake viongozi Afrika tawi la Tanzania, Dk Gertrude Mongella akizungumza kwenye mkutano wa leo jijini Dodoma.

 Washiriki mbalimbali wa Mkutano was Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika tawi la Tanzania leo jijini Dodoma. Uzinduzi wa mtandao huo utafanyika kesho ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mama Samia Suluhu Hassan.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...