Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAMIA ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa ngazi mbalimbali walio kazini na wastaafu katika Serikali zilizopita wameshiriki kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Baishara katika Serikali ya Awamu ya Tatu marehemu Mzee Iddi Mohamed Simba.

Mzee Simba amezikwa leo Februari 14,2020 katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu jijini Dar es Salaam ambapo wakati wa mazishi hayo , Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais mstaafu Mohamed Ghalib Bilali na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi Abdulrhaman Kinana ni miongoni mwa walioshiriki kwenye mazishi hayo.

Mwili wa marehemu Iddi Simba kabla ya kupelekwa makaburini, ulioshwa katika Msikiti wa Maamur na kisha kupelekwa nyumbani kwake eneo la Mikocheni nyumba kitalu namba 109.Baada ya hapo mwili wake ulikwenda kupumzishwa kwenye makaburi hayo baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa.

Baadhi ya viongozi wamepata nafasi ya kumuelezea na kwamba enzi za uhai wake alikuwa mstari wa mbele kutoa mchango wake mkubwa kwa Taifa letu kuhakikisha linasonga mbele kimaendeleo.

Kwa upande wake aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam katika Serikali ya Awamu ya Nne Suleiman Kova amesema mzee Iddi Simba baada ya kustaafu nafasi ya Uwaziri bado aliendelea kutumia muda wake mwingi kushauri na kushiriki bega kwa bega katika shughuli za maendeleo.

Amesema kifo chake ni pigo kubwa lakini cha kujifunza ni kuangalia sifa zake lukuki ambazo zimeelezwa na waombolezaji na waliobaki hai wana kila nafasi ya kujiuliza mwisho wao utakuaje ili kuwa mfano mzuri kama aliouachwa na marehemu Iddi Simba.

"Kuna mengi ambayo yamefanywa na Iddi Simba enzi za uhai wake, sifa zake tumezisikia zikitolewa na watu ambao wamepata nafasi ya kumzungumzia, alikuwa mzalendo na mwenye mapenzi mema na nchi yetu, "amesema Kova.


WASIFU WA IDDI SIMBA

Iddi Simba alizaliwa Oktoba 8 mwaka 1935 na aliingia kwenye siasa mwaka 1993. Baadaye alichaguliwa kuwa Mbunge wa Ilala jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alipata elimu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo Chuo Kikuu cha Punjab, Pakistani na Chuo Kikuu cha Toulouse nchini Ufaransa.

Pia Simba amewahi kuwa Mkurugenzi katika benki mbalimbali za kimataifa ikiwamo Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki mwaka 1968-1978.

Mwaka 1978-1980, Iddi Simba alikuwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika jijini Abijan, Ivory Coast. Pia amewahi kufanya kazi Benki ya Dunia nchini Marekani na Redio Tanzania.

Kwa nchini Tanzania Idd Simba amewahi kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango katika Wizara ya Uchumi na Mipango na Waziri wa Viwanda na Biashara.

Hata hivyo inaelezwa pamoja na kushika nafasi zote hizo, bado mzee Iddi Simba aliishi maisha ya kawaida na alikuwa mtu wa dini sana. Alipenda ndugu zake na watu wengine. Kutokana na kuwa mtu wa dini enzi za uhai wake aliteuliwa kuwa Mshauri wa Mambo ya Dini katika Msikiti wa Mtoro na Msikiti wa Manyema. Pia alikuwa mlezi wa klabu maarufu ya wana Dar es salaam ya Saigoni.

Marehemu ameacha mke aitwaye Khadija Simba na watoto wanne, ambapo wa kiume ni mmoja na watatu wakike watatu, akiwemo mwanahabari maarufu, Sauda Simba.  Pia ameacha wajukuu sita.
Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Benjamin William Mkapa (wa pili kushoto) na Dkt Jakaya Mrisho Kiwete na wakiwemo viongozi wa ngazi mbalimbali na wastaafu katika Serikali zilizopita wameshiriki kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu marehemu Mzee Iddi Simba.










Add caption







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...