Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga,
akitoa maagizo kwa Meneja Wa TANROADS, Mkoa wa Mbeya, Mhandisi
Eliazary Rweikiza (kulia), alipokuwa akikagua barabara ya Isyonje- Makete
(Km 96.4). Barabara hiyo inaunganisha mkoa wa Mbeya na Njombe.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga,
akifafanua jambo kwa kwa wawakilishi wa Mkandarasi M/s China Railway
Seventh Group wanaojenga barabara ya Njombe- Ndulamo – Makete
sehemu ya Moronga – Makete (Km 53.5).
 Muonekano wa barabara ya Njombe- Ndulamo – Makete sehemu ya
Moronga – Makete (Km 53.5). Barabara hii inajengwa kwa kiwango cha
lami na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group ambapo kwa sasa
imefika zaidi ya asilimia 48 na inatarajiwa kukamilika mwakani.
Mtambo wa kuchakata kokoto wa mkandarasi M/s China Railway Seventh
Group ukiwa eneo la mradi. Mkandarasi huyo anajenga barabara ya
Njombe- Ndulamo – Makete sehemu ya Moronga – Makete (Km 53.5).
PICHA NA WUUM.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga,
amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),
Mkoa wa Mbeya, kuhakikisha ndani ya siku mbili anakarabati maeneo yote
korofi yaliothiriwa na mvua katika barabara ya Isyonje- Makete (Km 96.4) ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.

Mwakalinga, ametoa agizo hilo mkoani Mbeya wakati alipokuwa akikagua
athari za mvua katika miundombinu ya barabara hiyo inayounganisha
mkoa wa Mbeya na Njombe akiwa katika kijiji cha Igoma, ambapo
amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwani ni kiungo cha mawasiliano
kati ya mikoa hiyo miwili.

“Hakikisha Meneja, barabara hii inapitika ifikapo kesho, kusanya
wataalamu wako wote waliopo katika mkoa wako, mje hapa kufanya kazi ili
kuhakikisha barabara hii inarudi katika hali yake ya awali” amesema
Mwakalinga.

Amesisitiza kuwa licha ya mvua kuendelea kunyesha katika baadhi ya
maeneo lakini bado wananchi wanahitaji hali nzuri ya barabara ili
kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao kutoka
sehemu mbalimbali.

Mwakalinga, amefafanua kuwa ameamua kufanya ziara hiyo ili kubaini
athari za mvua katika miundombinu ya barabara na kutatua changamoto
zake pamoja na kuangalia maendeleo ya miundombinu hiyo katika
maeneo mbalimbali nchini ili kuzipa kipaumbele katika kuzitengea fedha
barabara zote zenye changamoto kwenye bajeti ijayo.

“Kama mnavyojua kipindi cha bajeti kimekaribia, sasa ni muhimu kuzikagua
barabara hizi ili nione namna ya kuzipa kipaumbele kwa kuziwekea fedha
katika bajeti ijayo kwa barabara zote ambazo zina changamoto”,
amefafanua Mwakalinga.

Kwa upande wake, Meneja Wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi
Eliazary Rweikiza, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa atakarabati

kwa wakati barabara hiyo na kuhakikisha inapitika majira yote ambapo
ameongeza kuwa tayari mkandarasi ameshaaanza kurekebisha sehemu
zilizoharibika na kwamba ndani ya siku mbili kazi zote zitakuwa
zimekamilika na barabara kupitika.

Katika hatua nyingine, Mwakalinga, amekagua barabara ya Njombe-
Ndulamo – Makete sehemu ya Moronga – Makete (Km 53.5) ambayo
inajengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi M/s China Railway
Seventh Group.

Mwakalinga, amemtaka Mkandarasi huyo kuendelea na ujenzi kwa kazi
ambazo zinaweza kufanyika katika kipindi hiki cha mvua ili mradi ukamilike
kwa muda uliopangwa kulingana na mkataba.

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe, Mhandisi Yusufu
Mazana, amemhakikisha Mwakalinga kuwa atamsimamia mkandarasi huyo
ili aweze kukamilisha kwa wakati kwani mradi huo ni muhimu katika
usafirshaji wa mazao ya misitu, chakula pamoja na utalii.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...