Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius
Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Igis
anayesimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga –
Mpanda sehemu ya Koga – Kasinde (Km 112), mkoani Katavi.

Mkandarasi kutoka kampuni ya China
Wu Yi, Mhandisi David Kipiki, akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo,
Elius Mwakalinga (WaTatu Kulia), alipokuwa akikagua Daraja la Mto Koga,
mkoani Katavi.

Mhandisi kutoka Kampuni ya Egis,
akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga,
alipokuwa akikagua barabara ya Tabora – Koga – Mpanda sehemu ya Koga –
Kasinde (Km 112) , mkoani Katavi.

Muonekano wa Mtambo wa kuchakata
kokoto za ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda sehemu ya Koga –
Kasinde (Km 112), ukiwa eneo la mradi.

Muonekano wa barabara ya Tabora –
Koga – Mpanda sehemu ya Koga – Kasinde (Km 112), mkoani Katavi. Mradi
umefikia asilimia 56.5 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka
huu.
PICHA NA WUUM
……………………………………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mkadiriaji Majenzi, Elius
Mwakalinga, amewataka makandarasi wanaojenga miradi ya barabara nchini
kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ili kuweza kupata
taarifa za hali ya hewa zitakazowasaidia kupanga ratiba zao katika
utekelezaji wa miradi yao.
Kauli hiyo ameitoa mkoani Katavi
wakati akikagua barabara ya Tabora – Koga – Mpanda sehemu ya Koga –
Kasinde yenye urefu wa kilometa 112 ambapo amesema kuwa kupata takwimu
sahihi kutoka mamlaka hiyo kutasaidia kufanikisha miradi hiyo kwa
wakati.
“Hakikisheni mnatumia Mamalaka ya
Hali ya Hewa ili kujua majira ya mvua na kujiwekea mpango wa utekelezaji
wa miradi yenu, miradi mingi inashindwa kukamilika kwa muda uliopangwa
kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vipindi vya mvua kama ilivyo kwa
ukanda huu”, amesema Mwakalinga.
Adha, Mwakalinga amefafanua kuwa
kuhusu suala la madeni, Serikali itahakikisha inalipa kwa wakati madeni
yote ambayo makandarasi wanadai mara baada ya kuwasilisha nyaraka zao
na kuhakikiwa na Taasisi husika.
“Naahidi kufuatilia suala la malipo ambalo mmenieleza, na nitahakikisha kulipa fedha mnazodai kwani fedha zipo, kikubwa ni kuwasilisha hati sahihi ya madai kwetu”, amesema Katibu Mkuu Mwakalinga.
Mwakalinga, amempongeza mkandarasi
China Wu Yi anayejenga sehemu hiyo kwa kuajiri vijana wengi wazalendo
na kukubali kuchukua wataalam wanne kutoka wizarani ambao atawapatia
ujuzi kwenye mradi huo.
“Hakika nyinyi mmeonesha utofauti kati yenu na makandarasi wengine, sijawahi kuona mradi ulioajiri wazawa wengi kama huu, hakika hili ni suala la kufurahisha na kutia moyo”, amefafanua Katibu Mkuu Mwakalinga.
Kwa upande wake mkandarasi kutoka
kampuni ya China Wu Yi, Mhandisi David Kipiki, amesema kuwa
watahakikisha wanatekeleza mradi huo kwa ubora na kwa haraka ambapo
wanatarajia kukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Ameongeza kuwa mradi umefika
asilimia 56.5 na kwa sasa kazi zinazotekelezwa ni pamoja na uwekaji wa
lami katika baadhi ya maeneo ambapo kwa sasa jumla ya kilometa 29.5
zimeshawekwa lami.
Naye, Mhandisi Mshauri wa mradi
huo, Sidney Bishi, amemhakikishia Mwakalinga kuwa mradi huo utakamilika
kwa wakati kwani changamoto walizonazo hazitaweza kuzuia mradi
kutekelezeka na kumaliza kwa wakati.
Katibu Mkuu Ujenzi yupo mkoani
Katavi katika ziara ya kiakazi ambapo pamoja na mambo mengine amekagua
mradi wa Ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda (Km 328) ambapo
ujenzi wake umegawanywa sehemu nne ambazo ni Usesule- Komanga (km 112),
Komanga – Kasinde (112) na Kasinde- Mpanda (Km 104).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...