Na Karama Kenyunko Globu ya Jamii

MWANDISHI maarufu wa Habari za uchunguzi Erick Kabendera amehukumiwa kulipa faini na Fidia ya jumla ya sh. Milioni 273 baada ya kukiri makosa ya utakatishaji fedha na kukwepa kodi.
Aidha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Kabendera kulipa faini ya sh.250,000 ama kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela baada ya kukiri kosa la kukwepa kodi huku pia akifutiwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Hata hivyo mshtakiwa Kabendera ameishalipa Sh. Milioni 100 na kiasi kilichobakia cha sh. Milioni 173 atatakiwa kulipa kwa awamu katika kipindi cha miezi sita kuanzia leo Februari 24,2020.
Hatua hiyo imekuja baada ya mshtakiwa Kabendera  kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ya kuomba msamaha na kukiri makosa ya uhujumu uchumi yaliyokuwa yakimkabili.
Hukumu hiyo imesomwa leo Februari 24,mwaka 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega ambapo akisoma adhabu hiyo katika kosa la kwanza la ukwepaji kodi mshtakiwa ametakiwa kulipa faini ya Sh. 250,000 au kifungo cha miezi mitatu jela pia atatakiwa kulipa fidia ya Sh. Milioni 173.
Hakimu Mtega alisema katika kosa la pili la utakatishaji fedha mshitakiwa Kabendera atatakiwa kulipa faini ya sh. Milioni 100 na kusisitiza kuwa adhabu hizo zitakwenda peke yake.
Kutokana na adhabu hiyo Kabendera amelipa faini ya sh. 250,000 na anatakiwa kulipa kiasi cha Sh.Milioni 273 ambapo tayari ameshalipa kiasi cha sh. Milioni 100 na kiasi cha Milioni 173 kukilipa  ndani ya miezi 6 kuanzia leo.

KABENDERA YUKO HURU 
Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai mtuhumiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na hawana kumbukumbu  ya makosa ya nyuma hivyo, aliomba mahakama itoe adhabu kulingana na makubaliano yaliyofanyika.
Kwa upande wake, Wakili wa Mshitakiwa huyo, Jebra Kambole alidai kuwa kukiri makosa yake kumeipunguzia muda mahakama kuendesha mashitaka, ana familia na ndugu wanaomtegemea pia ni zaidi ya miezi sita sasa amekaa maabusu.
Alidai pia mshitakiwa huyo hali yake ya kiafya sio nzuri na wanaomba katika kosa la kwanza aweze kupewa faini ya sh. 250,000 kwa mujibu wa sheria ya kodi  na kwa kosa la pili aweze kupewa faini pia kwa mujibu wa sheria.
Mapema, akisoma makubaliano ya mshitakiwa huyo na DPP, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon alidai kuwa wameingia makubaliano na mshtakiwa huyo baada ya kukiri kosa la utakatishaji fedha na ukwepaji kodi hivyo DPP ameamua kumeondolea kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Baada ya kusoma makubaliano hayo, Hakimu Mtega alimuapisha mshtakiwa na kumuuliza  kama alisaini kwa hiari yake na kudai alifanya hivyo kwa hiari yake.
Miongoni mwa maelezo ya awali yaliyosomwa ni kuwa kati ya Januari Mosi, 2010 na Julai 29,2019 mshitakiwa alijihusisha na genge la uhalifu kwa kuingia mikataba isiyo halali na watu wengine ambao wapo nje ya Tanzania ikiwemo watu maarufu ambao hawapo mahakamani ambapo anadaiwa kukubali kufanya makosa ikiwemo kughushi, kukwepa kodi na utakatishaji fedha ambayo yanachangia kudidimiza uchumi.
Nchimbi alidai Machi 23, 2010 na kampuni yake iliyosajiliwa kama Voxy Media Center (T) Ltd na Wakala wa Usajili (Brela) na kwamba Januari 11, 2016 mshitakiwa pamoja na mkewe Loy Kabendera ambaye anajulikana pia Loyce Nganga walisajili kampuni ya Sitrep Company Limited na katika usajili huo waligushi fomu mbalimbali na kuonesha ofisi ya kampuni hiyo inapatikana kwenye nyuma namba 13 kitalu namba 23 Mbweni Mpiji Kinondoni ambayo ni nyumba yao ya kuishi.
Alidai mshitakiwa huyo pia katika mkakati wake wa kiuhalifu alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Serikali kwa lengo la kuidanganya serikali na kujipatia fedha kwa njia ya uhalifu.
Imedaiwa April 2, mwaka 2016  mshitakiwa huyo pamoja na mkewe walifungua akaunti mbili za fedha katika benki ya CRDB moja ikiwa ya fedha za kigeni, pia mshitakiwa alifungua akaunti yake binafsi na Januari Mosi, 2015 alipokea USD 230,358.83 kutoka kwa washitakiwa wenzake kupitia akaunti yake binafsi ambazo zilitoka kwa watu mbalimbali ikiwemo kampuni ya K2 Intelligence Ltd, Palladium (Tanzania) Ltd, Sitrep Co. Ltd, Eurasia Group Ltd, International Crisis Rou na taasisi zingine za kigeni.
Nchimbi alidai, Januari Mosi, 2015 na Agosti 29, 2019 mshitakiwa na mkewe Loy wakiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Sitrep walipokea USD 432,000,541 na Paundi 119, 000,130 na katika kipindi chote hicho hawakuwai kulipa kodi kwaTRA.
Hata hivyo Nchimbi alidai kuwa mshitakiwa huyo aliwaambia maofisa wa Polisi kuwa ajapokea fedha zozote kinyume na taratibu kutoka katika vyanzo visivyohalali.
Aidha uchunguzi wa awali ulionesha mshitakiwa huyo alijihusisha na shughuli za kihalifu na kufuatia uchunguzi huo alifunguliwa mashitaka mbele ya mahakama hii ambayo aliyakiri  kuyafanya.
Katika mashtaka mapya, imedaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi, 2015 na Agosti 29,2019  kipindi hicho, Kabendera alikwepa kodi kiasi cha Sh.173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe TRA.

Pia katika shitaka la pili, Kabendera anadaiwa alitakatisha Sh 173,247047.02 huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la ukwepaji kodi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...