Mkuu wa mkoa wa Mara Adam
Malima akimuonesha sehemu ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la hospitali
ya Rufaa ya Kwangwa Musoma Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara kukagua ujenzi wa hospitali
hiyo jana, Jengo hilo linajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua sehemu za jengo la
hospitali ya Rufaa ya Kwangwa alipofanya ziara kukagua maendeleo ya
ujenzi huo jana. Ujenzi wa jengo hilo unafanywa na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC). (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
………………………………………………………
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka
Shirika la Nyumba la Tiafa (NHC) kuongeza kasi ya ujenzi wa Hospitali ya
Rufaa ya Kwangwa iliyopo Musoma mkoa wa Mara ili kukamilika kwa muda
uliopangwa.
Hospitali hiyo ya
Kwangwa ni ya ghorofa tano yenye shemu tatu (Wing A, B na C) na
inarajiwa kuanza kutoa Huduma kwa baadhi ya sehemu kati kati ya mwezi
ujao
Dkt Mabula alitoa
kauli hiyo jana tarehe 25 Februari mjini Musoma mkoa wa Mara wakati wa
ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo unaofanywa na NHC akiwa
katika ziara yake ya siku moja.
Alisema, pamoja
na NHC kufanya vizuri katika ujenzi wa jengo la hospitali hiyo
ukilinganisha na wakandarasi waliotangulia lakini inapaswa kuongeza kasi
ili likamilike katika muda uliopangwa na kuanza kutoa huduma.
Kwa mujibu wa
Mabula, Hospitali ya Kwangwa itakayojulikana kwa jina la Mwl Nyerere
Memorial Hospital ina historia ndefu kwa kuwa pamoja na kuasisiwa na
Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Nyerere lakini utekelezaji wake
unakamilishwa na serikali ya awamu ya tano.
‘’Ni vyema NHC
mkaongeza bidii katika ujenzi wa hospitali hii ili ikamilike kwa haraka
kwa kuwa hospitali hii ina historia ndefu na Rais John Pombe Magufuli
ameamua ujenzi huu ukamilike kwa kutoa bilioni 15’’ alisema Mabula.
Katika
kuhakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati, Naibu
Waziri Mabula alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa NHC Dkt Maulid Banyani
kusimamia kwa karibu maendeleo ya ujenzi huo sambamba na kupatiwa ratiba
ya mpango wa ujenzi na maendeleo yake kila baada ya siku mbili kwa nia
ya kufuatilia kwa karibu.
Hata hivyo,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Dkt Maulid Banyani
alimuahakikishia Naibu Waziri Mabula kuwa, ujenzi wa hospitali hiyo sasa
utakamilika kwa wakati baada ya changamoto kadhaa ikiwemo ya Mshauri
Mwelekezi kupatiwa ufumbuzi.
Kwa Upande wake
Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima mbali na kuisifu NHC kwa kufanya
mabadiliko makubwa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa hospitali ya
Kwangwa alioueleza kuwa ilikwamwa kwa mara kadhaa.
‘’Toka Shirika la
Nyumba la Taifa lianze ujenzi wa hospitali hii mwezi Agosti mwaka jana
kuna mabadiliko makubwa ya kasi ya ujenzi na tunataka mjenge kwa
wakati na viwango na Machi mwaka huu Huduma ya Mama na Mtoto ianze
kutolewa ‘’ alisema Malima.
Kwa mujibu wa
Mkuu wa Mkoa wa Mara, hospitali hiyo itatoa huduma kwa wananchi wa mikoa
ya Kanda ya ziwa pamoja na nchi jirani sambamba na kutumika kama sehemu
ya utalii kutokana na mazingira ya hospitali.
Historia ya
Ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa iliyopo Musoma mkoa wa Mara inaanzia
mwaka 1977 pale Rais wa kwanza wa Mwl Nyerere alipotoa wazo la kujengwa
kwake lakini ujenzi huo umekuwa ukikwama kwa nyakati tofauti hadi Rais
John Pombe Magufuli alipotoa Shilingi Bilioni 15 kwa lengo la
kukamilishwa mradi huo ambapo sasa unatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...