Dare Es Salaam, 14 Februari 2020

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuwaondoa hofu na taharuki Watanzania hususan wazazi, ndugu na jamaa wa wanafunzi takribani 420 walioko katika jimbo la Hubei, mji wa Wuhan Nchini China, ambapo ndio kitovu cha maambukizi ya virusi vya homa ya Corona (COVID-19) kuwa hadi sasa hakuna mwanafunzi au Mtanzania yeyote aliyebainika kuambukizwa virusi hivyo na kuwasihi kuendelea kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kufuatilia hali zao kwa karibu.

Aidha,Wizara inapenda kuuhakikishia uma kwamba Serikali ya Tanzania haina mpango wa kuwaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao walioko Wuhan kwa kuwa wako katika uangalizi maalum (quarantine)nchini humo kutokana na serikali kuheshimu masharti na mahitaji ya karantini hiyo yanayozuia mtu yeyote kutoka ama kuingia katika mji huo kwa kusudi la kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo hadi hapo Serikali ya China itakapoondoa karantini hiyo.

Uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutowaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao kurejea nyumbani unatokana  na taarifa za kitabibu zinazobainisha kutokea milipuko ya homa ya virusi hivyo katika mataifa ambayo awali yaliwaondoa wananchi wao wakati wa mlipuko na kusababisha kusambaa kwa virusi hivyo na kuleta madhara zaidi kwa mataifa hayo.

Serikali inawasihi Wazazi,ndugu na jamaa wa wanafunzi hao kuwa watulivu na kuepuka kutumika kisiasa katika suala hili la Virusi vya Corona kwani magonjwa hayana siasa na Virusi hivi ni hatari kwa mtu yeyote na vinasambaa kwa kasi.


Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wake uliopo Beijing imeendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali kupitia Mawasiliano ya moja kwa moja na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na Ofisi za Kimataifa za Vyuo Vikuu walipo Wanafunzi kutoka Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwapatia vifaa vya kinga ikiwemo viziba pua (Masks) na sabuni maalum za kunawa mikono (Disinfecants) pamoja na kusaidia utatuzi wa mahitaji ya lazima pale inapojitokeza.

Tayari Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewasiliana kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi kuhusu hali za Watanzania ambaye amemhakikishia usalama wao.

Serikali pia inakamilisha mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia za simu (hotline) zitakazotumiwa na wataalamu wa saikolojia (psycho-social support) kwa ajili ya kuwapatia ushauri nasaha wanafunzi na wazazi wakati juhudi za kudhibiti mlipuko huo zikiendelea.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaishukuru Serikali ya Watu wa China kwa hatua na juhudi zinazoendelea kukabiliana na virusi hivyo na kutoa wito kwa Mataifa mengine duniani kusaidia jitihada za China kutokomeza ugonjwa huo. 

Mwisho, Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu hali za Watanzania waliopo nchini China hususani katika jimbo la Hubei na mji wa Wuhan na kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto zitakazojitokeza katika kipindi hiki.

China ilikumbwa na mlipuko wa homa ya corona (the novel coronavirus- 2019-nCoVambavyo jina lake rasmi kwa sasa kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni COVID – 19 kuanzia Januari, 2020.

  
Emmanuel Buhohela
Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...