MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemkuta Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Zitto Kabwe kupitia tiketi ya chama cha ACT- Wazalendo anayekabiliwa na kesi yake ya uchochezi ana kesi  ya kujibu

Hatua hiyo imefikiwa leo Februari 18 2020  na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kufuatia Wakili wa Serikali Tumaini Kweka kudai mahakamani hapo kuwa upande wa mashitaka umefunga ushahidi katika kesi hiyo kufuatia kuita mashahidi 15

Akitoa uamuzi huo Hakimu Shaidi amesema, amepitia ushahidi wote uliotolewa na mashahidi upande wa mashtaka na kuona mshtakiwa ana kesi ya kujibu, hivyo atatakiwa kujitetea.

Kufuatia taarifa hiyo Zitto ambaye anatetewa na Wakili Jebra Kambole  amedai atajitetea kwa njia ya kiapo na ataanza kujitetea Marchi 17 hadi 20  mwaka huu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Marchi 17,18,19 na 20 mwaka huu.

Mapema, Wakili wa Serikali Kweka alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya uamuzi lakini wanataka kufahamu kwa nini mshitakiwa Zitto hakufika mahakamani Februari 10 mwaka huu wakati kesi yake ilipokuja kwa ajili ya uamuzi.

Akijibu hoja hiyo, Zitto alidai kuwa alikuwa anaumwa na alitoa barua za hospitalini kudhibitisha juu ya kuugua kwake.

Hata hivyo upande wa mashitaka ulidai kuwa hawaielewi barua hiyo ndipo Zitto aliwajibu kuwa waende ubalozi wa Marekani kujiridhisha.

Katika kesi ya msingi Zitto anakabiliwa na mashitaka matatu ya uchochezi ambapo, anadaiwa Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Inadaiwa kuwa mshitakiwa alitamka kuwa ‘’…watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na Polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua..’’

Katika shitaka la pili ilidaiwa Oktoba 28, mwaka huu maeneo ya Kijitonyama katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’…lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya, ni taarifa ambazo zinaonesha wananchi wengi sana wameuawa na jeshi la Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi…kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kisheria za kuchukua na sio kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa…’’

Ilidaiwa kuwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’… Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na Polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi…’’

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...