Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amewaambia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu na tayari kuna watu wameanza kujipitisha kwenye kata na majimbo kabla ya wakati, hivyo ametoa onyo kwa yoyote anayejipitisha mapema atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya Chama hicho.
Mama Samia ameyasema hayo leo Februari 13,2020 kwenye mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam. Mkutano huo ulihudhuria na wanachama wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa Chama hicho ngazi ya Mkoa .
"Mwaka huu unaitwa kumekucha na kweli kumekucha, kila mmoja sasa amekaza buti , amekaza mguu lakini nawaombeni sana fuateni miongozo yetu ya Chama inavyotuongoza.Kuna watu wameanza kujipitisha mapema kwenye majimbo na hao majina yao tunayo.Tayari kuna fedha zinatoka, tayari kuna takrima zinatoka lakini nataka niwaambie, jicho la Chama, jicho la Serikali liko wazi na linawaona.
"Kama wewe ni mchezaji subiri filimbi ipigwe halafu wote muanze kucheza, usianze kucheza halafu filimbi ikipigwa wewe unaweka mpira goloni. Nataka kuwaambia tunanao marefa wazuri wanaofuatilia, ukianza kucheza rafu tutaona na mimi kama mlezi naomba niwaambie hili lipo na tunawaona, watu wameanza kampeni mapema,"amesema Mama Samia.
Amefafanua wabunge bado wako katika majimbo yao wakiendelea kutimiza majukumu yao na hata wakionekana majimboni ni sehemu ya kutekeleza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi."Lakini wewe ambaye sio Mbunge ukienda na fedha zako lazima tuhoji, kwanini uende sasa, wenzenu wabunge wameanza kazi ya kutumikia majimbo yao muda mrefu, subirini wakati ufike, mwenye uwezo anajulikana na asiye na uwezo anajulikana".
Pia amesema katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi kuna viongoziBwameanza kutumika, na baadhi yao wanahusika kuwasimamisha wanachamaambao wanawaona ni tishio kwao.
 Kuna watu wanasimamishwa hovyo hovyo uko chini , ukiangalia sababu unakuta tu mamlaka ya maeneo huska na wanafanya hivyo kwa kumhofia kuwa atakuwa tishio mbele ya safari.Chama chetu kina utaratibu wa kuchukua hatua , hivyo lazima miongono na kanuni ifuatwe.Nilikuwa mkali sana na Kamati ya siasa Mkoa, nikawauliza kwanini hali hii wakasema wanaofanya hivyo wanatumia madaraka waliyonayo huko chini, hivyo kamati ya siasa ya mkoa inayo nafasi ya kusimamia.
"Msitupunguzie mtaji mapema hivyo, kila ambaye mnamfukuza ana ndugu na rafiki, kwanini mtengeneze nongwa sasa hivi, ndugu zangu uchaguzi uliopita fimbo tulijipiga wenyewe, watu wanatosha , tunasema hawatoshi, watu wakakatwa tu hovyo hovyo, wengine wakanuna wakaenda upande wa pili.Wengine walienda wakaturahibia,"amesema.
Wakati huo huo Mama Samia amesema kama wewe ni mwana CCM kindaki ndaki ni vema ukafuata kanuni na sheria za Chama pale ambapo unahisi umetendewa ndivyo sivyo badala ya kwenda upinzani na kuanza kushirikiana nao ili kuharibu.
"Wengi wenye itikadi za CCM pamoja na kupatwa na changamoto bado walibaki na tukashirikiana nao vizuri.Hawa wenye tabia ya kujiengua sio wenzetu na vema tukawabaini mapema,"amesema.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...