***************************

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amempeleka Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo eneo inapojengwa shule maalumu ya wasichana itakayojulikana kama Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge inayojengwa katika eneo la Kikombo Jijini Dodoma

Akiwa katika eneo hilo la ujenzi Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai amesema ni vyema Waziri anayehusika na uendeshaji na usimamizi wa shule akajua mapema sehemu inapojengwa na mendeleo ya ujenzi wake ili kama kuna maboresho aweze kuyatoa mapema na kufanyiwa kazi.

“Hapa tunajengwa kwa kutumia ‘Force Account’ mfumo ule ule ulioasisiwa na TAMISEMI na ramani za majengo ni zile zile za TAMISEMI ila kuna baadhi ya maeneo tumeboresha kidogo lakini hatujaenda nje ya maelekezo ya Wizara hii kuhusu ujenzi wa miundombinu ya shule” Alisema Spika Mhe. Ndugai.

Akizungumzia wazo wa kujenga shule hiyo Spika Ndugai alisema Waheshimiwa Wabunge Walifanya changisho kupitia matukio ya kijamii na wadau mbalimbali wakachangia jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 1.2 fedha hiyo ilipatikana kutoka katika sehemu ya posho za Wabunge na michango ya wadau hao.

“Lengo la awali ilikua kujenga vyoo vya mfano vya wasichana katika kila Jimbo Nchini lakini baadae tukaona tuunganishe nguvu tujenge kitu kimoja kikubwa kitakachoacha alama ya Bunge la 11 mara litakapomaliza muda wake”.

Hakika katika hili Bunge la 11 limefanya kazi ya zaida, zaidi ya ile ambayo tumeizoea na ipo Kisheria ambayo ni kutunga Sheria wakati huu tumeamua tufanya kazi ya Jamii itakayoboresha Elimu ya mtoto wa Kike wa Tanzania na tukaelekeza nguvu katika ujenzi wa shule hii ya mfano ya Wasichana alisema Spika Ndugai.

“Shule hii inayojengwa itakua na miundombinu yote inayohitajika kwa ajili ya Shule ya Sekondari kuanzia madarasa ya kutosha, maabara, mabweni, bwalo la kisasa, vyoo, ofisi za walimu, jengo la utawala pamoja na library yenye miundombinu ya TEHAMA” aliongeza Spika Ndugai.

Aidha Spika Ndugai ameweka wazi kuwa ujenzi wa shule hiyo utakamilika Mwezi Juni, 2020 na kwa umoja wa Bunge la 11 wataikabidhi kwa Waziri wa TAMISEMI Mhe. Jafo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Joseph Magufuli.

Akizungumza akiwa katika eneo la ujenzi wa shule hiyo Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amemshukuru Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai pamoja na Wabunge wote wa Bunge la 11 kwa michango yao na wazo lenye tija la kujenga shule maalumu ya Wasichana ya Bunge.

“Nimefarijika sana kuaona wazo hili limeanza kutekelezwa na ndoto ya Bunge la 11 sasa inaanza kutimia na kwa sababu Spika amekuja kunionyesha kuanzia leo na mimi nitakuwa napita mara kwa mara kuangalia maendeleo ya ujenzi huu ili kwa pamoja tuweze kuikamilisha ndoto hii ya Bunge letu” Alisema Jafo.

Nitahakikisha kuwa Shule hii mara inapokamilika na kukabidhiwa TAMISEMI tunapanga walimu wenye ubora na wanafunzi wenye ufaulu mzuri ili kwa pamoja waweze kuleta matokeo mazuri ya shule hii, tunakata shule hii iwe ya mfano na maalumu kwa heshima ya Bunge la 11 alisema Jafo.

“Tunataka tuienzi shule hii kwa heshima ya Bunge la 11 tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanafunzi watakaosoma hapa wanafaulu kwa viwango vya juu ili shule hii iweze kuingia katika shule kumi bora za Tanzania katika matokeo ya kidato cha sita alisisitiza Jafo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...