Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi imeihakikishia dunia kwamba uchaguzi mkuu ujao, utakuwa huru na wa haki.

Kabudi ameyasema hayo kwenye hafla ya kukaribisha mwaka mpya ambapo amekariri ahadi ya Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo aliyoitoa akizihakikishia jumuiya za kimataifa kuhusiana na suala hilo. Akizungumza na mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa jijini Dar es Salaam Kabudi amesema: 
“Mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa sita tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa na uchaguzi huo utakuwa wa uwazi, huru na wa haki.” Ameongeza kwamba, Tanzania itawaalika waangalizi wa uchaguzi watakaotaka kushuhudia namna Watanzania wanavyotekeleza moja ya haki zao za msingi katika suala la kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wao.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Tanzania ametoa kauli hiyo katika hali ambayo, kilio kikubwa cha vyama vya siasa ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, vikisema kuwa mfumo wa sasa wa tume iliopo unawapa mamlaka wakurugenzi kusimamia uchaguzi wakati ni wateule wa Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala cha CCM.
 Aidha akihutubia kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi Waziri Kabudi pia alisema serikali ya Tanzania inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote za binadamu zikiwemo za kisiasa na kwamba sheria zilizotungwa na bunge la nchi hiyo zina lengo jema la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Taifa lenye amani, umoja na utulivu. 
Alizidi kufafanua kuwa, madai yanayotolewa dhidi ya Tanzania kuwa inakiuka haki za binadamu ni propaganda zinatokana na hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, dawa za kulevya, uzembe katika ofisi za umma pamoja na hatua zinazochukuliwa kulinda rasilimali za Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...