* Snura, Juma Nature watoa ujumbe kwa wakazi wa Dar, Pwani

Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
TUME ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imesema imeridhishwa na muamko wa wananchi katika mikoa yote ambao wameuonesha kwenye uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Kwa mujibu wa NEC Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani walikuwa wamepewa fursa hiyo ya kujiandikisha kuanzia Februari 14 hadi Februari 20 mwaka huu ambapo wananchi wengi wa mikoa hiyo wamejitokeza huku wale ambao bado hawajiandikisha waende kujiandikisha.

Akizungumza na Michuzi Gobu na Michuzi TV, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura Giveness Aswile wakati wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha iliyoambatana na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii nchini, amesema mchakato wa kuandikisha wapiga kura wapya, waliopoteza vitambulisho, waliohama makazi na waliokuwa wanataka kuuhuhisha taarifa zao limekwenda vizuri katika maeneo yote ambayo NEC imepita.

Aswile amesema NEC imevuka lengo ambalo ilikuwa imejiwekea katika mchakato huo wa kuwapatia wananchi kitambulisho cha mpiga kura wakiwemo wale ambao wametimiza umri wa miaka 18 au Oktoba mwaka huu watakuwa na umri huo.

Amesema kwa Dar es Salaam na Pwani kazi ya andikishaji unaendelea na muamko ni mkubwa sana kwani wengi wamejiandikisha."Tunaomba wale ambao bado hawajajiandikisha wakatumia nafasi hii maana Februari 20 mwaka huu ndio mwisho wa uandikishaji."

Kwa upande wake Msanii Snura Mushi maarufu Snura amesema ni muhimu wananchi kuwa na kitambulisho cha mpiga kura ili kupata fursa ya kuchagua viongozi wanaowahitaji kwa maendeleo ya nchi yetu.

"Kitambulisho cha mpiga kura ni muhimu sana, licha ya baadhi yetu kukichukulia poa, kitambulisho cha mpiga kura ni muhimu kwa taifa letu.Ukiwa na kitambulisho hiki utakuwa na nafasi ya kuchagua kiongozi ambaye unaamini atatufaa kwa ajili ya maendeleo yetu au kuendelea kumchagua ili kuendelea kuleta maendeleo. Naomba wananchi tutumie nafasi hii kupata kitambulisho cha mpiga kura,"amesema Snura.

Wakati huo huo msanii Juma Kassim a.k.a Juma Nature amewasisitiza wananachi wa Wilaya ya Temeke na maeneo mengine ya Dar es Salaam kwenda kujiandikisha kwenye daftari hilo kwani ni muhimu kutumia nafasi hiyo iliyotolewa na NEC."Chonde chonde ndugu zangu naomba tukajiandikishe."

Baadhi ya wananchi ambao wamefika kwenye kampeni hiyo ya kuhamasisha kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura, wameipongeza NEC kwa uhamasishaji ambao wameufanya kwani utasaidia hata wale ambao bado hawajajiandikisha kwenda kwenye vituo kujiandikisha.
 Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura Giveness Aswile(kushoto) akimtunza Msanii Snura Mushi wakati wa tamasha la kampeni ya kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura.Kampeni hiyo imefanyika viwanja vya Mwembe Yanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye kampeni ya kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wakiwa na vitambulisho vyao wakati wa kampeni hiyo iliyofanyika Mwembe Yanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
 Msanii Snura Mushi maarufu kwa jina la Snura akiendelea kutoa burudani wakati wa tamasha la kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
 Msanii Juma Kassim a.k.a Juma Nature akitoa burudani wakati wa kampeni ya kuhamasisha wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
 Snura Mushi akicheza moja ya nyimbo zake wakati wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
 Waanchi wakiwa katika Viwanja vya Mwembe Yanga wakifuatilia burudani na matangazo ya kuwahamasisha kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura .Kampeni hiyo imeandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC).
 Baadhi ya wananchi wakicheza nyimbo ya Snura wakati wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
 Msanii Snura Mushi akiendelea kusakata muziki mbele ya wananchi wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye kampeni ya kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...