Mdhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu mwenye suti ya Kaki akitoka mahakama baada shauri lao maombi yao kuomba mahakam itoe amri ya kumkamata kuahirishwa. Kushoto ni wakili wake Nyaronyo Kicheele

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mjini, Tundu Lisu umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwapatia muda wa wiki mbili (Siku 14 ) kwa ajili ya  kupitia na kuchambua maombi ya wadhamini wa mshtakiwa Lissu.

Wadhamini hao leo Februari 21,2020 kwa nyakati tofauti wameileza mahakama kuwa wamewasilisha maombi mahakamani hapo kuomba itoe hati ya kukamatwa kwake ili waweze kujitoa udhamini kwa sababu  mtuhumiwa huyo hahudhurii katika kesi yake.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amekiri kupokea maombi ya wadhamini hayo yakiambatanishwa na hati ya kiapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kuomba Mahakama iwapatie muda wa kutosha waweze kuchambua maombi hayo.

"Mheshimiwa ni kweli tumepokea hati ya kiapo cha maombi ya wadhamini, tunaomba mahakama itupatie muda wa kutosha ili tuweze kuchambua maombi hayo kwa sababu maombi hayo yana vitu vingi hivyo mheshimiwa tunaomba utupangie tarehe nyingine" alisema Simon.

Akijibu hoja hiyo Hakimu Simba amewapatia upande wa mashtaka muda wa siku 14 huku akiwasisitiza watumie siku 10 kuhakiki maombi hayo kabla ya kurejea mahakamani.

Mapema hakimu Simba amewataka wadhamini kueleza alipo mshtakiwa Lisu kwa kuwa walishakiri kwamba amepona na mahakama ilihitaji kumuona akihudhuria kesi.

Mmoja wa wadhamini hao Robert Katula amedai kuwa ni kweli alisema mshtakiwa amepona ila walipojaribu kuwasiliana naye ili aje mahakamani alidai ana wasiwasi na usalama wa maisha yake na ndiyo sababu ameomba mahakama ishughulikie maombi yao.

Kabla ya hakimu kupanga tarehe wakili Simon alidai kuwa mshtakiwa namba mbili katika kesi hiyo Simon Mkina hakuonekana mahakamani kwa siku mbili bila taarifa akaiomba mahakama itakaporudi mshitakiwa aonywe na na wadhamini wake watoe maelezo ni kwa nini mshtakiwa huyo hakuhudhuria mahakamani.

Akijibu hoja hiyo Wakili wa utetezi Nyaronyo Kicheere amedai kuwa siku ya jana Mshtakiwa Mkina alifika lakini aliumwa ghafla akalazimika kurudi nyumbani na bado hali yake si nzuri.

Hakimu Simba ameendelea kusisitiza wadhamini wa Lisu kumleta mahakamani hapo kwani kwani amri za kesi hiyo bado zinaendelea mpaka zitakapotenguliwa baadaye.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Machi 10, 2020.
Lisu na wenzake wanne katika kesi ya msingi wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo  kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa kati ya  Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...