Na Ripota Wetu Kongwa .

WILAYA  Kongwa imewataka wajasiriamali kuzingatia mafunzo yanayotolewa na Serikali pamoja na taasisi zake yenye lengo la kuboresha bidhaa wanazozizalisha, kukuza mitaji yao na hatimaye kupata uhakika wa soko la bidhaa.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kongwa, Audiphace Mushi, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo,  Deogratius Ndenjembi, wakati akifungua mafunzo kwa wazalishaji wa mafuta ya alizeti na wauzaji wa bidhaa za chakula na dawa katika ukumbi wa Halmashauri  ya Mji mdogo wa Kibaigwa, wilayani hapa.

Mushi alisema washiriki watumie fursa hii kuelewa masuala  mbalimbali yanayofundishwa ili watakapomaliza wakawe mabalozi wazuri kwa wale ambao hawakupata fursa ya kushiriki katika mafunzo haya yenye lengo la kuwataka wazalishaji kufuata taratibu na Sheria za nchi zilizopo.

“Serikali ya sasa inatutaka tufuate utaratibu ili kuepuka matatizo mbalimbali, mafunzo haya yawe ni chachu ili kuwafikia wengine,”alisisitiza Mushi na kuongeza kuwa wanapaswa kuwa wadadisi ili waweze kupata manufaa yatokanayo na mafunzo haya na hatimaye waweze kuboresha bidhaa zao ziweze kupatiwa alama ya ubora na kuweza kumudu ushindani katika soko.

Vilevile, aliwasisitiza washiriki kuwa mabalozi kuhusu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na mafunzo waliyopata kwa ujumla, kwani ubora na viwango ni jambo lisilokwepeka katika dunia ya sasa.

Alisema TBS imefanya uamuzi mzuri kuandaa mafunzo katika Halmashauri ya mji  mdogo wa Kibaigwa kwani mji huu ndiyo kitovu cha wazalishaji wa mafuta ya alizeti na wauzaji wa bidhaa za chakula na vipodozi na ni mara ya kwanza kwa TBS kufanya mafunzo ya aina hii na TBS inatakiwa kufanya tathmini ya mafunzo kwa wadau waliopatiwa mafunzo.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika mafunzo haya, Meneja  Utafiti  na Mafunzo wa  TBS, Hamisi Sudi alisema suala la mafunzo ni miongoni mwa majukumu makuu ya Shirika yenye lengo la kuweka uelewa wa pamoja kwa wazalishaji nchini juu ya masuala ya  viwango.

Sudi alisema kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Shirika ,Iimefanya mafunzo kama haya katika kanda ya Magharibi iliyohusisha wilaya za Kigoma,Kibondo,Kasulu na Katavi; Kanda ya Ziwa katika wilaya za Bukoba, Geita, Bariadi na Kahama  na sasa  Kanda ya Kati katika wilaya za Iramba, Singida, Manyoni,Kondoa, Kongwa na Dodoma.

Alisema pia katika mwaka huu wa fedha pia Shirika litatoa  mafunzo katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kaskazini.

Katika  mafunzo haya  yanayotolewa  na TBS kuhusu  masuala ya viwango pia hushirikisha wadau kutoka Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), maafisa Afya, Biashara  na Maendeleo ya Jamii kutoka katika wilaya husika.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya  Kongwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Audiphace Mushi  (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na  washiriki wa mafunzo, wakufunzi kutoka TBS, SIDO   na Halmashauri ya wilaya ya Kongwa,  baada ya ufunguzi rasmi ya mafunzo ya wazalishaji wa bidhaa za mafuta ya alizeti na wauzaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi inayofanyika leo katika ukumbi wa Hamashauri ya Mji  Mdogo wa Kibaigwa wilayani hapa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...