Na Mwandishi  Wetu, Singida

WAZALISHAJI wa bidhaa mbalimbali mkoani Singida wametakiwa kutambua kuwa suala la viwango ni la kisheria hivyo ni lazima kuthibitisha ubora wa bidhaa ili kumlinda mlaji na kupata uhakika wa soko la bidhaa wanazozizalisha.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu  wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt Rehema Nchimbi alipokuwa akifungua mafunzo ya wazalishaji wa bidhaa za vyakula yakiwemo mafuta ya alizeti na wauzaji wa vipodozi na vyakula yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA  mkoani Singida.

Dkt. Nchimbi alisema suala la ubora wa bidhaa linapaswa kuzingatiwa katika mnyororo wote wa uzalishaji ili  mlaji awe salama  na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutozingatia viwango.

“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ndiyo hakikisho la wazalishaji na fursa zinazotengenezwa zitakuwa dhahiri iwapo masuala ya viwango yatazingatiwa, vilevile TBS ni daraja kati ya mzalishaji na soko, hivyo mzalishaji ni lazima kufuata utaratibu,” alisisitiza Dkt. Nchimbi.

Alisema maisha  ya binadamu ni chakula hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wake, kwani bidhaa  hafifu zinagharimu afya ya walaji  na kwamba magonjwa mengi yanatokana na jinsi tunavyoandaa chakula na tunavyokula, hivyo wazalishaji wanapaswa kuwa waaminifu katika kuzalisha bidhaa yoyote.

Dkt. Nchimbi alisema TBS siyo adui  wazalishaji hawapaswi kuichukia na wajenge dhana kuwa TBS ni usama hivyo wazalishaji wa Singida wahakikishe kuwa wanazalisha bidhaa bora wakati wote ili kudhidhirisha kauli kwamba Singida ni njema wakati wote.

Akizungumzia kwa upande wa TBS, Dkt. Nchimbi alisema Shirika  linapaswa kuangalia namna ya kuongea na wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa yale wanayowafundisha wanaelewa kikamilifu. Mafunzo haya yawe na kipimo ili kujua kama yameeleweka vizuri na kwamba watakaopokea  mafunzo ndiyo watakaowapima.

Kwa upande wake Meneja wa  Mafunzo na Utafiti kutoka TBS, Hamisi Sudi alisema Shirika litaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa kwa kuzingatia viwango.

Alisema Shirika linatambua  kuwa wajasiriamali wana mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi walio wengi hivyo Shirika lina mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa jamii hasa wajasiriamali kwakuwa ni mojawapo ya majukumu yake ya kila siku.

Shirika likiwa mkoani Singida limetoa mafunzo kwa wajasiriamali 221 Katika wilaya za Iramba, Singida na Manyoni, ambayo pia yamewashirikisha watendaji wa Halmashauri wakiwemo maafisa Biashara, Maendeleo ya Jamii na Afya pamoja na Maafisa kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

Pia Shirika linatarajia kutoa mafunzo katika wilaya za Kondoa, Kongwa na ikiwa ni muendelezo wa mafunzo katika Kanda ya Kati.
 Mkuu wa Mkoa wa  Singida, Mhe.Dkt.Rehema Nchimbi (aliyeketi katikati)akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo maalum kwa wazalishaji wa mafuta ya alizeti pamoja na wauzaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi, mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa VETA mkoani Singida, wengine walioketi kulia  ni Afisa Biashara wa mkoa wa Singida Bw.Daniel Munyi, wa pili kutoka kulia ni Meneja wa Mafunzo na Utafiti kutoka TBS, Bw. Hamisi Sudi, kushoto ni Meneja wa SIDO Singida, Bi Agnes Yeseya na wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Meneja wa Mkanda ya Kati - TBS Bw. Sileja Lushibika.
 Baadhi ya washiriki katika mafunzo mkoani Singida
 Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora  naMeneja wa Mafunzo na utafiti, Bw. Hamisi Sudi Akisoma hotuba ya Ukaribisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya kabla ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi kufungua mafunzo ya siku moja kwa wazalishaji wa mafuta ya alizeti na wauzaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA mkoani hapa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...