Veronica Simba – Pwani
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imewasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Kisemvule, kilichopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Tukio hilo lilifanyika Machi 17 mwaka huu, wakati Kamati hiyo ikiwa katika ziara kukagua miradi ya umeme vijijini mkoani Pwani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Vedastus Mathayo, aliwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa ya uwepo wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) katika eneo hilo kutokana na gharama yake nafuu ya shilingi 27,000 tu.

“Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuwaletea umeme huu wa gharama nafuu. Changamkieni fursa, mlipie kwa wingi ili kila mmoja aunganishiwe huduma hii kwa ajili ya kujiletea maendeleo.”

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika Wilaya ya Mkuranga kwa Kamati, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alisema mpaka sasa vijiji 44 kati ya 125 vimekwishapelekewa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa kwanza.

Alieleza zaidi kuwa, kwa kutambua umuhimu wa nishati ya umeme kwa wananchi na kwa namna Wilaya hiyo inavyokua kwa kasi, Serikali iliamua kuongeza wigo wa Mradi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwamba kazi inaendelea.

“Katika wigo wa awali, Mkandarasi alikuwa ameshaunganisha wateja 6,000. Mahitaji yakawa makubwa, Serikali ikaongeza wateja wapya takribani 4,000 na kazi inaendelea,” alieleza Naibu Waziri.

Alisema kuwa, matarajio ya Serikali hadi ifikapo Juni mwakani, maeneo yote yawe yamefikiwa na umeme kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza mkoani Pwani utanufaisha vijiji 150 ambapo mpaka sasa vijiji 115 tayari vimekwishawashiwa umeme.

Aidha, mbali na mradi wau meme vijijini, iko miradi mingine ya umeme inayoendelea kutekelezwa mkoani humo ikihusisha Peri-Urban, Ujazilizi (Densification) na miradi mingine inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
 Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Vedastus Mathayo (mwenye mkasi), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Kisemvule, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, Machi 17, 2020. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
 Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Vedastus Mathayo, akibofya king’ora maalum kuashiria kuwasha rasmi umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Kisemvule, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, Machi 17, 2020. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga na mwenye ushungi ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
 Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akitoa salamu za ukaribisho kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ilipotembelea Kijiji cha Kisemvule na kuwasha umeme katika Zahanati yake, Machi 17, 2020. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Vedastus Mathayo na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga.
 Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga akitoa salamu za ukaribisho kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ilipotembelea Kijiji cha Kisemvule na kuwasha umeme katika Zahanati yake, Machi 17, 2020.
 Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ally Kessy akiwa mbele ya Zahanati ya kijiji cha Kisemvule, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani. Kamati husika iliwasha rasmi umeme katika Zahanati hiyo, Machi 17 mwaka huu wakiwa katika ziara ya kazi kukagua miradi ya umeme vijijini.
 Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiwa katika hafla ya uwashaji umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Kisemvule, Mkuranga, mkoani Pwani, Machi 17 mwaka huu.


 Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji cha Kisemvule, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, wakifuatilia hafla ya uwashaji rasmi umeme katika Zahanati ya kijiji hicho, uliofanywa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), Machi 17 mwaka huu.
 Sehemu ya umati wa wananchi wa Kijiji cha Kisemvule, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani wakitawanyika baada ya kushuhudia uwashaji rasmi umeme katika Zahanati ya Kijiji hicho, uliofanywa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Machi 17 mwaka huu.
Afisa wa Bunge kutoka Wizara ya Nishati, Alex Nduye (kushoto) na Katibu wa Naibu Waziri wa Nishati, Mhandisi Ngereja Mgejwa, wakijadiliana jambo wakati wa hafla ya uwashaji umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Kisemvule, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, uliofanywa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), Machi 17 mwaka huu.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...