Mstahiki Meya wa Halmashauri ya
Manispaa ya Kinondoni katikati Mhe. Benjamini Sitta akiwa na Naibu Meya
George Manyama na Kaimu Mkurugenzi Dk. Patricia Henjewele wakiwa katka
kikao cha robo ya pili cha baraza la madiwani.

Mbunge wa jimbo la Kinondoni, Mhe.
Maulid Mtulia akizungumza wakati wa kikao cha robo ya pili cha Baraza
la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa.

Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Kinondoni, Nasoro Shemzigwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo katika baraza la madiwani lililofanyika katika
ukumbi wa manispaa hiyo.
****************************
Baraza la
madiwani Manispaa ya Kinondoni limepongeza wakala wa Barabara Mijini na
Vijijini (TARURA) kwa usimamizi na ukaratabati mzuri wa barabara
zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Pongezi hizo
zimetolewa katika kikao cha kawaida cha robo ya pili cha baraza la
madiwani ambapo madiwani hao wameeleza kuwa TARURA imefanya kazi kubwa
ya kutengeneza barabara katika maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri
hiyo na hivyo kuwezesha mitaa mbalimbali kuwa na muonekano mzuri.
Awali Meneja wa
TARURA wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Leopold Runji alisema kuwa mtandao
wa barabara katika Manispaa hiyo ni kilomita 1700 ambapo hadi sasa Km.
170 zimejengwa kwa kiwango cha lami, Km. 390 zimejengwa kwa kiwango cha
changarawe (Moram) huku Km. 1140 katika kiwango cha vumbi kwa
kusawazishwa na Greda.
Mhandisi Runji
alifafanua kuwa mkakati wa TARURA kwa barabara za vumbi ambazo
hazijafikiwa na huduma ya ukarabati kwa maeneo ya Kata na Mitaa
mbalimbali zimewekwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021 ambapo zaidi ya
Km. 197 zitafanyiwa ukarabati huo.
Katika hatua
nyingine Baraza hizo limepitisha taarifa mbalimbali za kamati za kudumu
za Halmashauri hiyo zilizowasilishwa na wenyeviti ambapo kamati hizo ni
Uchumi, Afya na Elimu, Kamati ya Mipango miji ujenzi na mazingira,
Kamati ya Maadili, Kamati ya Ukimwi pamoja na Kamati ya fedha na
uongozi.
Awali akisoma
Taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya
pili ya mwaka , Kaimu Mkurugenzi Dk. Patricia Henjewele alisema kuwa
katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020, Halmashauri ilikisia
kukusanya na kupokea kiasi cha sh. Bil.150.6 ambapo kati ya fedha hizo
Tsh. Bil. 110.5 ni ruzuku kutoka Serikali kuu na Tsh. Bil. 40. ni fedha
za makusanyo ya ndani.
Kuhusu miradi ya
maendeleo, Dk. Henjewele alieleza kuwa katika mwaka wa fedha wa
2019/2020, Halmashauri hiyo ilikisia kutumia kiasi cha Tsh. Bil.81.5
kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na
vyanzo mbalimbali vya mapato pamoja na nguvu za jamii.
Alivitaja vyanzo
hivyo vya fedha kuwa ni Tsh. Bil. 19.8 zinatokana na mapato ya ndani na
kiasi cha Tsh. Bil. 61. 5 ni ruzuku kutoka Serikali kuu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...