*Ni Athony Komu ambaye sasa anaitwa msaliti, muongo
*Atoboa siri ya kamati ya watu sita iliyohusika kwa Lisu

Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii

MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro Anthony Komu(Chadema) amekiri amewahi kuwa na tofauti na viongozi wa ngazi za juu wa Chama hicho na aliamini hayo ni mambo ya kawaida kwa taasisi kubwa na inayokuwa.

Kwa bahati mbaya kuwa na mtazamo tofauti na wenzie kwa kiwango kikubwa umechukuliwa kuwa uasi ndani ya chama jambo linalosababisha kutoaminika hata ple ambapo angeweza kutoa mchango mzuri wa kusaidia kujiimarisha.

Komu amesema imefika mahali amekuwa akiitwa majina mengi tu yakiwemo ya msaliti, muasi, mwoga, na mroho wa madaraka na wapo ambao walikuwa wakimtabiria kuwa anataka kwenda CCM kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano lakini ameweka wazi kuwa licha ya kwamba ataondoka Chadema baada ya muda wake wa ubunge kumalizika na kujiunga na NCCR-Mageuzi ambako anatarajia kugombea ubunge kupitia Chama hicho kwenye Jimbo la Moshi Vijijini ambalo kwa sasa yeye ndio mbunge wake.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Komu amewaambia waandishi wa habari kuwa kiini cha kuitwa majina yote hayo yanatokana tu na sababu za kutofautaiana na wenzake katika baadhi ya mambo na hasa uendeshaji wa Chama hicho , jinsi ya kukiongoza kimuundo, namna ya kupanga nafasi mbalimbali ndani ya Chama na vipaumbele vyao katika azma ya kushika Dola.

"Kwa muda mrefu nimenyamaza ili wanaofahamu ukweli wanisemee , bahati mbaya waliojaribu kinisemea nao walituhumiwa na vita ya maneno ikawa kubwa.La kujiuliza ni je yote haya ni kwa faida ya nani? Na ni kwanini tumekuwa watunzi wa riawaya na waoiga ramli?"Alihoji Komu.

Amesema kuwa mfano mzuri wa kutoaminika hata pale baadhi yao wanapopata fursa au uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya Chama inakuwa vigumu kupewa ushirikiano ni matibabu ya Tundu Lisu na kwamba mara tu baada ya Lisu kufikishwa Nairobi baada ya jaribio la kutaka kuuliwa alipata ushauri toka kwa Mtanzania anayeishi nchini Ubelgiji kuwa wafanye kila linalowezekana wamhamishie huko kwa kuwa zipo fursa za kuweza kupata matibabu bora zaidi na ya uhakika kutokana na maendeleo makubwa ya kiteknolojia na hata kwa gharama nafuu mara dufu.

"Kwa kuwa nilimfahamu mtu huyo vizuri nilifanya safari kwenda Nairobi kumshauri Mwenyekiti wao (Freeman Mbwe) kuhusu fursa hiyo.Mbowe alihoji mambo ya msingi sana ikiwa ni pamoja na uendelevu wa matibabu yenyewe , uangalizi wa mgonjwa hasa ukizingatia umbali kati ya Dar es Salaam na Ubelgiji , hadhi ya hospitali na suala zima la usalama.Yote haya tuliyafanyia kazi kwa kuunda kamati ya watu sita huru akiwemo Mbunge wa Ubungo Said Kubenea na wengine walitoka nje ya Chama chetu.

"Tukaamua kujitolea kufanikisha upatikanaji wa taarifa hizo kwa uhakika;zote zilipatikana ikiwa pamoja na kwenda mkapaka Ubelgiji kuona hospitali iliyokusudiwa na kupata uhakika wa usalama wa Lisu akiwa huko.Nikaziwasilisha kwa Mwenyekiti bado maneno yaliendelea eti tunatumiwa na Serikali kupitia mume wa huyo Mtanzania.Baadhi ya vijana walionekana kutumwa sijui kwa ajili ya kumpeleka Lisu Ubelgiji kwa kisingizio cha matibabu bora na nafuu zaidi ili aweze kuhudhuria kirahisi.Ulitengenezwa uongo mkubwa hata wa kuhusisha raia wa nchi jirani kuwa watatumika na Serikali kumuangamiza.

"Baada ya kujiridhisha kuwa nia zetu ni safi na kuombwa na kutiwa moyo na dugu zake wawili , ndugu Alute kaka yake mkubwa na Vicent ambaye ni mdogo wake ambaye alikuwa mmoja ya wanakamati ya watu sita , tuliamua kuyapuuza na bila msaada wowote wa Chama tulipambana ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha za kutanguliza hospitali zilihitajika kama Shilingi 114,000,000, kilipia bima ya kuanzia usafiri wake na wasaidizi wake na ni wapi wangeishi wakati wakimuuguza .Tukafanikisha bahati njema naye Lisu alipopata fahamu naye akachagua njia hiyo , hivyo ikashindikana kutuzuia,"amesema Komu wakati anatoa taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Ameongeza kuwa pamoja na ukweli huo mpaka leo Lisu yuko salama na hapajawahi kutokea tishio lolote la usalama wake na kwa zaidi ya miaka miwili aliyokaa hospitali nchini Ubelgiji akipewa matibabu ya hali ya juu Chama na wasamaria wema hawajawahi kudaiwa hata shilingi moja na kwamba katika miezi minne ambayo Lisu alikuwa Nairobi Chama chao kikilipa Sh.700,000,000.

Komu amesema hata hivyo pamoja na jitihada zote hizo na ukweli kuwa mpango huo umekiondolea Chama mzigo mkubwa sana wa gharama , bado wapo baadhi ya viongozi wakubwa wanaondelea kumuandama yeye pamoja na Kubenea kwamba walitumia shambulio la Lisu kujitafutia umaarufu wa kisiasa na kumhujumu Mwenyekiti wao.

"Haya yote yanayoendelea yanafahamika ndani ya Chama ,lakini hakuna hatua zozote za maksudi zinazochukuliwa na uongozi wa Chama kusahihisha au kufafanua jambo hili, ili mbegu ya chuki iliyopandwa dhidi yetu na ambayo imezalisha majina kama usaliti isiendeleee kushamiri , hali hii ya viongozi wangu kunyamazia hatua za aina hii imenihuzunisha na kunikwaza sana.

"Bahati mbaya jitihada za kutaka kuondokana a halii na ili tubaki tukiwa wamoja tunapoelekea uchaguzi mkuu zinaonekana zimeshindakana .Kwa mtazamo wangu na uzoefu kuwa mpinzani ni sawa na kuwa na vita dhidi ya watawala, silaha moja muhimu ni kuwa wamoja na kuaminiana, kwa sasa nikiri dhana nzima ya kupendana na kuaminiana imeondoka na badala yake tunatuhumiana , tunabaguana na kujengeana uadui dhidi yetu wenyewe.

"Hali hii imeongezeka zaidi baada ya uchaguzi wa ndani ya Chama ambao umekiacha Chama na majeraha makubwa yanayohitaji tiba; bila hivyo madhara yake ni mabaya .Aidha malumbano haya yametuondoa katika ajenda zetu za msingi kama vile ushirikiano wa vyama na madai ya Katiba mpya ambayo iliunganisha wapinzani wote na makundi mengine muhimu.

"Leo inaonesha wazi kuwa tumeanza kuondoka katika ajenga hiyo.Kiongozi mmoja wa dini aliniuliza mbona ninyi mnajipendelea? Mmeamua kudai Tume huru ya uchaguzi kwa kuwa inawahusu?Nikajitetea mpaka kwa maneno ya Nkurumah kuwa tupate kwanza uhuru wa kisiasa mengine yatafuata,"amesema.

Amefafanua kuwa ujumbe hapo ni kwamba kiongozi huyo wa dini anawaambia wameacha agenda za wananchi , wameacha kuwaratibu au wameshindwa kuratibu matatizo yao.Hivyo wameanza kusahau vipaumbele vya watu kama watawala.Wanahabari wanataka kuona agenda zao zikiendelezwa mfano sheria ya magazeti , makosa ya mtandaoni, kila mmoja angependa eneo lake lipewe uzito wa kwanza.

"Wapo wanaoona marekebisho ya kwanza yanayotakiwa kufanywa ni kwenye sheria ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, wengine muundo wa muungano na kero zake , wengine madai ya uwepo wa Mahakama ya Kadhi na wengine mamlaka ya Rais.Kwa maoni yangu malumbano yetu wenyewe yanatuondoa kwenye wajibu wetu wa kuwaunganisha Watanzania katika kudai mazingira bora zaidi kwenye kila nyanja ambalo jukumu letu la msingi kama wapinzania,"amesema Komu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...