Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii

MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Anthony Komu(Chadema) amtengaza rasmi baada ya muda wake wa ubunge kumalizika kwa mujibu wa sheria basi ataachana na Chama hicho na kisha kujiunga na NCCR-Mageuzi ambacho ndicho atatumia kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Mbali na kutangaza msimamo wake wa kuondoka Chadema wakati utakapofika, komu ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua kwa hatua mwenendo wake wa kisiasa ndani ya Chadema ambao uaonesha kwa sehemu kubwa hana furaha kutokana na kuitwa msaliti, kutengwa na wakati mwingine akituhumiwa kuwa anasuka mpango wa kumpindua Mwenyekiti wao Freeman Mbowe.

Akizungumza leo Machi 29 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam Komu amesema msimamo huo ameutoa mapema kwa manufaa mapana ya upinzani na kwamba itaondoa majungu yanayoendelea kwa kisingizio labda anataka ahakikishiwe kuteuliwa kugombea ubunge tena kupitia Chadema au anataka kurudi katika nafasi ya ukurugenzi wa fedha.

"Huu ni utamaduni mzuri ambao ni vema ukaigwa na wengine ambao wanayo mipango yao mfukoni tofauti na ile vyama vyao. Mimi nimeiga utaratibu huu kwa wenzetu wa Kenya ambapo Naibu Rais wa Kenya William Ruto ametangaza kuwa katika uchaguzi ujao wa 2022 atagombea lakini sio kwa Chama chake cha sasa.

"Ni imani yangu kuwa Chama changu cha Chadema kitalichukua suala hili kwa mtazamo chanya na kwa kuzingatia misingi tuliyojijengea wenyewe katika Katiba yetu na Sera zetu .Katiba ya CHADEMA toleo la 2016 sura ya nne kifungu 4.0(4.1.4)uk.8-9.Dhana ya uamuzi wangu umeelezwa vizuri kwa Maneno yanayosema kuhakikisha mtu ana uhuru wa kwenda mahali popote ndani ya mipaka ya nchi na anaweza kushirikiana na mtu yeyote ndani na nje ya nchi katika kuendeleza maslahi halali,"amesema Komu wakati atangaza uamuzi huo.

Pia amesema kuwa sera za Chadema zinasisitiza katika kifungu cha 1.2 kwa Maneno haya ;" ...Chadema itahakikisha kila mwananchi anakuwa na uhuru kamili wa kueleza fikra zake ,kupata na kutoa habari ,kukusanyika na kujiunga na kikundi au Chama chochote kwa hiari na utashi wake.Hivyo amesema uamuzi wake si wa kukurupuka wala wa kibabe bali amewashirikisha watu wengi kiasi na anaowaamini wana mapenzi mema na nchi.

"Na baadhi ya watu ambao nimeshauriana nao kwa namna moja au nyingine wamechangia katika mafanikio niliyoyapata katika harakati zangu za kisiasa, hao wanatoka kwenye familia yangu, taasisi za dini , asasi za kiraia , wanasiasa na wanaharakari huru wa ndani na nje,"amesema .

Amefafanua kuwa wengi ambao amezungumza nao wamempa baraka zote na kwamba anaomba kila mmoja atakayeguswa kwa namna yoyote na uamuzi huo auangane na waliompa baraka za kwenda mbele kwa kuwa wote wanajenga nyumba moja hivyo hakuna sababu ya kugombania fito.

Komu amesema anafahamu fika kwenye historia yake ya siasa hakuingizwa na mtu na wala hakumfuata mtu yoyote na kwamba alianza mageuzi kwa kuchagua kushindia juisi ya mua ya wapemba,akaacha kuajiriwa Serikalini licha ya wakati huo kutokuwa na changamoto za uhaba wa kupata ajira.

"Tulichagua kulala mbugani kwenye nyumba za tembe za wananchi badala ya mahotelini kwa kuwa tulijipa wajibu wa kubadilisha hii nchi ili mzawa aone matunda ya Uhuru na ndio maana tulianza na itikadi ya uzawa tukaendelea kubadilika mpaka tukakomea kwenye Utu.Baada ya kutafuta sehemu sahihi ya kufanya siasa tulikwenda kuanzisha NCCR-Mageuzi na huko tukajifunza kuwa uzawa unaweza kutafsiriwa kama ubaguzi, hivyo tukaboresha kwa kuweka utu na kuondoa uzawa,"amesema Komu.

Ameongeza kuwa anakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa wanachama wakikosa mabadiliko ndani ya CCM basi watayatafuta nje ya CCM , hivyo ni vema ushauri huo Chama chake cha sasa wakauzingatia."NCCR-Mageuzi ni sehemu sahihi kwangu pamoja na kupita kwenye changamoto kwa nyakati tofauti lakini wamebaki kuwa wamoja na hakuna mahali wanatupiana maneno ya kejeli na kubezana, hivyo nimeamua nitakwenda huko."

Amesema katika harakati za siasa aliamua kuondoka NCCR-Mageuzi na kwenda Chadema lakini baada ya kutafakari kwa kina mwenendo wa Chama hicho na namna kinavyoendeshwa ni wakati sahihi kwake kurudi NCCR -Mageuzi ambako anatarajia kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu atagombea ubunge kupitia Chama hicho.

"Kwanini nitarudi NCCR-Mageuzi , jibu ni kwamba kwanza ni itikadi yake ya utu, kwa maoni yangu tumeacha kuheshimiana , hivyo utu unatukumbusha kuwa sisi ni sawa na kila mmoja anastahili kutendewa sawa na mwingine .Pili ni utulivu na ukomavu uliopo NCCR-Mageuzi baada ya kupitia matatizo makubwa.

"Kihistoria baada ya uchaguzi mkuu mwaka 1995 ,NCCR-Mageuzi kiliibuka Chama kikuu cha upinzani nchini na tangu wakati huo kimekuwa chama ambacho kinaweza kuhimili changamoto za kisiasa hata pale kinapokuwa hakina mbunge.Kila uchaguzi kinashiriki na kinafanya vizuri , hivyo huko ni sehemu sahihi kwangu kwani naamini bado mchango wangu wa mawazo na kuwatumikia wananchi kuleta maendeleo bado ninao tena wenye ari kubwa,"amesema Komu.

Ameongeza kuwa kabla ya kuamua kuwa atakwenda NCCR-Mageuzi wakati utakapofika amefuatwa na vyama mbalimbali vya siasa lakini msimamo wake ni kwamba chama sahihi kwake kwa sasa ni hicho."Katika maisha yangu ya siasa pamoja na mambo mengine nimekuwa mstari wa mbele katika kuona wapinzani tunaungana na nilishiriki kwenye harakati zao kutaka Chadema kuungana na NCCR-Mageuzi ili tuwe na Chama kimoja ambacho kitafahamika kwa jina la Umoja wa Demokrasia Tanzania(UDETA), hata hivyo hatukuwa tumefanikiwa."
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Anthony Komu(Chadema) 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...