MNEC MWAKITINYA, TAASISI YA JASIRI ASILI WAWAPA ELIMU YA KUJITAMBUA WANAFUNZI SEKONDARI YA IHUMWA

Charles James, Michuzi TV
WANAFUNZI nchini wametakiwa kuepuka vishawishi vya kimahusiano na vyenye kuwapeleka kwenye utumiaji wa dawa za kulevya ili kuweza kutimiza ndoto zao.

Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), MNEC Mussa Mwakitinya wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ihumwa jijini Dodoma leo.

Mwakitinya ambaye ameambatana na Taasisi ya Jasiri Asili walifika katika shule hiyo kwa ajili ya kuzungumza na wanafunzi hao na kuwaeleza umuhimu wa elimu ya darasani na kujitambua.

Amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli imefanya pamoja na kufanya mambo makubwa kwenye sekta zote lakini uwepo wa sera ya elimu bila malipo umeleta manufaa makubwa sana kwa watoto wengi hasa wa familia maskini.

" Wadogo zangu mna nafasi kubwa kwenye hii Dunia, asiwepo mtu yoyote wa kuvuruga ndoto zenu kwa kuwahadaa kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kwani mtapata mimba za utotoni na mtashindwa kufikia ndoto zenu.

Siyo mimba tu kuna hatari ya kupata magonjwa ambukizi kama Ukimwi hivyo niwasihi muepuke vishawishi vyote na mkiona mnasumbuliwa sana toeni taarifa kwa wazazi, walimu na hata viongozi wa kiserikali wa Mtaa," Amesema MNEC Mwakitinya.

Amesema ni jambo la aibu kuona licha ya Rais Magufuli kulipa mabilioni ya fedha kwenye elimu ili wanafunzi wasome bado wanafunzi wanashindwa kusoma kwa bidii na kufaulu.

" Rais Magufuli amejitoa kwa ajili yenu ili msome, mna fursa ya kusomwa na wala hudaiwi karo kama zamani. Deni lenu ni moja tu kwa Rais nalo ni kufaulu vizuri na kuondoa historia mbaya ya shule yenu ambapo tangu ianzishwe mwaka 2007 imepata daraja la kwanza kwenye matokeo ya kidato cha nne mara mbili tu," Amesema Mwakitinya.

Nae Mwanzilishi wa Taasisi ya Jasiri Asili, Diana Msacky amesema malengo ya taasisi yao ni kutoa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi lengo likiwa kuwakumbusha umuhimu wa wanafunzi kujilinda na vishawishi vinavyowakumba.

Diana amesema changamoto kwa wanafunzi siyo kwa watoto wa kike pekee bali hata wa Kiume wamekua wakikumbana nazo ikiwemo za ulawiti na utumiaji wa dawa za kulevya.

" Hata wadogo zangu wa kiume msikubali kukaa kimya mtu anapowafanyia vitendo viovu vinavyoweza kuhatarisha afya zenu na ndoto zenu. Toeni taarifa pindi inapotokea mtu anakufanyia vitendo hivyo ili mamlaka za kisheria ziweze kuchukua hatua.

Lakini pia nimeona kwa kipindi cha mwaka mmoja wanafunzi watano wamepata ujauzito. Niwasihi sana muepuke kuingia kwenye mambo yanayoharibu ndoto zenu. Serikali inawapenda imewapa elimu bure jukumu lenu ni kusoma kwa bidii na kuhakikisha mnatimiza ndoto zenu," Amesema Diana.

Nae Mkuu wa Shule hiyo, Grayson Maige ameupongeza uongozi wa Jasiri Asili kwa kujitoa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule yake huku pia akimuahidi MNEC Mwakitinya kuwa kiwango cha ufaulu shuleni hapo kitaongezeka mwaka huu kwa kutoa daraja la kwanza.
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mussa Mwakitinya akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ihumwa iliyopo jijini Dodoma wakati alipoambatana na Taasisi ya Jasiri Asili kutoa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi hao.
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ihumwa wakifuatilia mkutano wao na Taasisi ya Jasiri Asili na MNEC wa CCM Taifa, Mussa Mwakitinya shuleni kwao jijini Dodoma.
 Mkuu wa Shule ya Sekondari Ihumwa jijini Dodoma, Mwalimu Greyson Maige akizungumza na wanafunzi wa shule yake kwenue mkutano wa pamoja wa kutoa elimu mbalimbali ikiwemo ya kujitambua ambayo imeandaliwa na Taasisi ya Jasiri Asili.
 MNEC wa CCM Taifa, Mussa Mwakitinya akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Ihumwa jijini Dodoma leo.
 Mwanzilishi wa Taasisi ya Jasiri Asili, Diana Msacky akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Ihumwa jijini Dodoma leo.
 Mwanzilishi wa kusaidia wanafunzi ya Jasiri Asili, Diana Msacky akizungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Ihumwa leo kuhusu umuhimu wa elimu na namna ya kujitambua ili kufanikisha ndoto zao.
 Wanafunzi na Walimu wa Shule ya Sekondari Ihumwa jijini Dodoma wakiwa kwenye mkutano wa pamoja na Taasisi ya kusaidia na kuelimisha wanafunzi ya Jasiri Asili ambayo pia iliambatana na Mjumbe wa NEC Taifa, Mussa Mwakitinya.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...