Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
MWENYEKITI wa Ngome ya Wanawake wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa Mkiwa Kimwanga ameikumbusha jamii na hasa ya wanawake wote nchini kuhakikisha wanawalinda watoto na ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Pia amesema wanaunga mkono tamko ambalo limetolewa na Kiongozi wa Chama hicho Zitto Kabwe kwa hatua ya kumuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli kwa kushauri Watanzania kuwa wamoja na kuchukua tahadhari kadri inavyowezekana ili kujieousha na virusi vya Corona.

Akizungumza leo Machi 30,mwaka 2020 jijini Dar es Salaam Kimwanga ambaye ameteuliwa kwenye nafasi hiyo siku za karibuni baada ya Chama hicho kufanya chaguzi zake za ndani, ameeleza kuwa ni wazi kwa sasa nchi mbalimbali duniani zinandelea kupambana na janga hilo ambalo limesababisha mamia ya watu kupoteza maisha.

Hivyo amesema kuwa kwa Tanzania Serikali imeonesha umakini kwa kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo ya kufunga shule zote kwa siku 30 ili wanafunzi warudi nyumbani.
"Sisi Ngome ya Wanawake wa ACT Wazalendo kwanza kabisa tunaunga mkono tamko la Kiogozi wetu wa Chama Zitto Kabwe hasa kwa barua yake ambayo ameiandika kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kutaka Watanzania kuwa wamoja na kuchukua tahadhari.

"Pili tangu ugonjwa huu kutangazwa kuna hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa ikiwemo ya kufunga shule za msingi, sekondari na vyuo kwa siku 30.Pia Serikali ilionesha umakini kwa kuhakikisha zinachukuliwa tahadhari za kujiepusha na ugonjwa huu,"amesema Kimwanga.
Akifafanua zaidi amesema tangu shule kufungwa kama hatua ya kukabiliana na janga la Corona , mitaani bado kuna watoto wengi ambao wamekuwa wakiranda randa na kuzurula, hivyo amewashauri na kuwambusha kuwa kufungwa kwa shule hizo maana yake wazazi hasa akina mama wanatakiwa kuchukua jukumu la kuwalinda watoto wasipate maambukizi ya Corona.

"Tuwe karibu na watoto na kuwafundisha jinsi gani wanaweza kuepuka maambukizi kama vile kuhimiza kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka.Tuwasiruhusu kwenda kuranda randa mtaani bila sababu kwani ni ngumu kujua huko aliko yuko kwenye hatari ya kupata maambukizi kwa kiwango gani.

"Pia tunafahamu walimu baada ya shule kufungwa waliamua kuwapa kazi za kufanya wanafunzi ili hata wakiwa nyumbani wawe na kazi ya kufanya ambazo zinahusu masomo yao.Ni wajibu wetu wanawake ambao ndio walezi kuhakikisha tunawakumbusha wanafunzi kufanya kazi ambazo wamepewa shuleni kwenye kipindi hiki ambacho wako nyumbani,"amesema Kimwanga na kubwa zaidi wawe makini kufuatilia mienendo ya watoto wao.
Ameongeza kuwa familia ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe pamoja na kuwa makini bado imekumbwa na tatizo la ugonjwa wa Corona na hiyo inaonesha ni kwa kiwango gani wazazi na walezi wanatakiwa kuwa makini zaidi kwa kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kwa watoto na familia kwa ujumla.
"Tuendelee kusikiliza maelekezo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto pamoja na viongozi wa Serikali wanasema nini katika kukabiliana na gonjwa hili hatari.Nitumie nafasi hii kuungana  na Kiongozi wetu wa Chama kuhusu ushauri wake kwa Wizara ya Afya wa kwamba kuwe na vifaa vingi vya kupima Corona ili wananchi wapate fursa ya kujitambua mapema,"amesema.
Pia amewaomba akina mama wa Ngome ya ACT Wazalendo kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kutoa elimu inayohusu umma kuchukua tahadhari, kwani Serikali imekuwa ikitoa elimu hiyo lakini wao kwa nafasi yao wanayo fursa ya kukutana na jamii iliyoko chini kabisa na kuendelea kukumbusha elimu inayotolewa na Wizara ya Afya.
Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa Mkiwa Kimwanga akisoma taarifa yake kwa waandishi wa habari leo Machi 30, mwaka 2020 jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa akina mama kubeba jukumu la kuwalinda watoto wasipate maambukizi ya virusi vya Corona katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...