NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
WANAFUNZI 320 wa shule ya sekondari ya Kata ya Mapinga wameondokana na kero ya ukosefu wa maji uliokuwa ukiwakabili,baada ya taasisi ya It’s Time To Help Foundation Tanzania ikishirikiana na Feza Schools Tanzania kutekeleza mradi wa uchimbaji kisima kilichogharimu mil.12.

Ofisa Uhusiano wa Taasisi hiyo, Mbwana Kitendo akizungumza kwenye makabidhiano ya mradi huo alisema, taasisi hiyo ina utaratibu wa kutoa misaada kwa jamii katika sekta za afya, elimu na ustawi wa jamii,pia hutoa misaada kwa vituo vinavyohudumia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
"Kutatua changamoto hii kwetu ni mafanikio makubwa kwani tunaamini
sasa wanafunzi watasoma kwa amani bila kufikiri tena changamoto ya
kukosa maji na hii itawaongezea utulivu na ubunifu katika masomo yao”
alieleza. Mbwana.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ,Julius
Mwanganda aliishukuru taasisi ya hiyo na kuwa tayari kutoa msaada huo
kwani ni ukweli usiopingika kuwa Shule hiyo ilikuwa na changamoto
kubwa ya ukosefu wa maji.

Alifafanua, hali hiyo iliyowaletea usumbufu mkubwa na kuwaondolea
utulivu wanafunzi hasa wa kike na si wanafunzi tu hata walimu kwani
maji ni huduma muhimu na ya msingi kwa mwanadamu yeyote mahali popote,hivyo utatuzi wa changamoto hii utaleta ufanisi mkubwa kielimu na
utendaji kazi kwa ujumla shuleni hapo.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Mapinga, Agnes Mmbaga
alisema awali walikuwa wakitumia maji toka katika kisima cha kuchimba
kwa mkono kilichochimbwa na walimu pembezoni mwa Shule hiyo, ambacho
hakikuwa na maji ya uhakika wala salama kiafya, hali hii ilipelekea
kupoteza muda mwingi kutafuta maji badala ya kutumia muda huo kwenye
masomo.

Alibainisha, mradi huo wa maji ni ukombozi kwa wanafunzi na walimu wa
Shule hiyo huku akiahidi kuutunza mradi huo ili uendelee kutoa huduma
hiyo muhimu kwa muda mrefu.

Mmbaga anaongeza, “Shule yetu hii ina changamoto nyingi ikiwemo
upungufu wa vyumba vya madarasa, uzio, umeme, maabara, maktaba,
matundu ya vyoo na Ofisi ya Walimu, hivyo nawaomba wadau wa elimu
kufika katika Shule yetu na kutusaidia kutatua changamoto hizi.

Shule mpya ya Sekondari Mapinga,ilianza kujengwa mapema mwaka 2019 kwa nguvu za wananchi, Halmashauri na wadau wa maendeleo katika Kata hiyo na ilipata usajili Mwezi Januari mwaka huu.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...