Issa Mtuwa – Dodoma
TIMU ya wataalam 9 kutoka Wizara ya Madini, Wiziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wiziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeundwa ili kumsaidia Mjasiliamali wa miaka 60 kutoka mkoani Njombe wilaya ya Ludewa, Reuben Mtitu maarufu Mzee Kisangani ili kutimiza ndoto yake ya kuwa bilionea baada ya kubuni  kiwanda kinachotengeneza zana zinazotokana na madini ya chuma. 

Kamati hiyo imeundwa leo tarehe Machi 30, 2020 na Mawaziri Wanne wa Wizara ya Madini Doto Biteko, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Zungu, OR-TAMISEMI Mwita Waitara na Naibu waziri ya Viwanda na Biashara Mhandisi, Stella Manyanya, katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wizara ya madini jijini Dodoma. Wengine waliohudhuria  ni kutoka Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), Mazingira (NEMC) na Wataalam kutoka wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Akifungua kikao hicho, Waziri Biteko amewaeleza wajumbe hao, kuwa lengo ni kujadili namna ya kumsaidia Mzee Kisangani kwenye kila hatua kutoka mahali alipo ili ikibidi awe bilionea.  Ameongeza kuwa, mzee Kisangani hajui kusoma wala kuandika lakini ameonyesha kitu ambacho kama Serikali inahitaji kumsaidia kwa kila hatua anayohitaji.

Biteko amesema, alipokuwa ziarani mkoani njombe kuanzia Machi 13-16, alitembelea kiwanda chake ambapo kwa namna kilivyo, lakini kinatengeneza zana mbalimbali za chuma kama vile, Mapanga, Fyekeo, Visu, Majembe huku akiwa amewaajiri watu 30, kutokana na uthubutu na juhudi alizonazo. Waziri Biteko akiwa ziarani katika eneo hilo aliahidi kukutana atakutana na Mawaziri wote wanao husiana na shughuli zake ili kujadili namna ya kumsaidia.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Zungu, akichangia namna ya kumsaidia, amesema wizara yake kupitia (NEMC) itahitaji andiko (Bussines Plan) na kwamba wataalam wa eneo hilo watasimama ipasavyo kusaidia Mzee Kisangani kufikia ndoto yake. Wakati Zungu akihitaji andiko, Biteko amesema tayari Chuo Kikuu cha Mzumbe walishajitolea kumuandikia andiko la biashara (Business Plan) ya kiwanda chake. Naye Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI Mwita Waitara, amesema kila mkoa ulipewa agizo la kuandaa maeneo ya uwekezaji hivyo Mkuu wa Mkoa mkoani humo atatoa eneo maalum kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha Kisangani kwenye eneo lililotengwa.

Kwa upande wake, Naibu wa Viwanda na Biashara Mhandisi, Stella Manyanya amesema kumekuwa na changamoto nyingi za kuwasaidia watu wenye ubunifu hususani kutokana na vipengele vilivyowekwa kisheria suala ambalo huwakatisha tamaa. 

Amesema wizara yake kupitia NDC, SIDO na TIRDO kila taasisi itatoa mtaalam kwa ajili ya kumsaidia mjasiliamali huyu ili afikie malengo.
Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi amesema mara baada ya kusoma taarifa za ziara ya waziri wa Madini kupitia vyombo vya habari alituma wataalam kwenda kiwandani hapo na kuona namna gani ya kumsaidia ili kuzalisha chuma na kuongeza uwezo wa uzalishaji. 

Waziri Biteko ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, amesema kwakuwa tunataka kuona matokeo ya huyu Mzee kutokana na nguvu za serikali ndipo iliamriwa kuundwa kwa kamati ya wataalam wa aina mbalimbali ambao ni wizara/taasisi kwenye mabano, Wilfred Machumu (Tume ya Madini), Issa Mtuwa (Wizara ya Madini), Abbas Mruma (GST), Prof.  Silvester Mpanduji (SIDO), Prof. Madundo Mtambo Mkumbukwa (TIRDO), Dr. Yohana Mtoni (NDC),  Anorld Mapinduzi (NEMC), Leo Mavuka (TAMISEMI), na Dr. Hellen (Chuo Kikuu Mzumbe. 
Waziri wa Madini Doto Biteko mwenye suweta na wananchi mbalimbali wakimsikiliza Reuben Mtitu maarufu Mzee Kisangani alipomtembelea kwenye kiwanda chake cha kutengeneza zana mbalimbali

Waziri wa Madini Doto Biteko Katikati akiongoza wajumbe wa wizara nne kwa ajili ya kumsaidia Reuben Mtitu maarufu Mzee Kisangani ambae ni Mjasiliamali kutoka wilayani Ludewa aliye azisha kiwanda cha kutengeneza zana za madini ya chuma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...