WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania kwa nafasi yake ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)imeendelea kupaza sauti ya kuondoa vikwazo kandamizi vya kiuchumi vilivyowekwa katika Jamhuri ya Zimbabwe.
Amesema
ili wasiache hata mmoja wao nyuma wanapoelekea kwenye utekelezaji wa
Ajenda ya SADC ya baada ya mwaka 2020 yaani SADC Post 2020 Agenda, ni
vyema wakaendelea kuisemea Zimbabwe katika majukwaa mbalimbali ya
Kikanda na Kimataifa hadi vikwazo hivyo vitakapoondolewa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Machi 18, 2020) wakati akifungua
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere,
jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umefanyika kwa mara ya kwanza kwa njia
ya kimtandao (video conference).
Amesema
kama ilivyokubalika katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali
na kongamano la kihistoria lililowakutanisha wadau wa Kitaifa na
Kimataifa na nchi rafiki kwa ajili ya kupaza sauti kwa kauli moja juu ya
nchi hiyo kuondolewa vikwazo, wanapaswa kuendelea hivyo hadi vikwazo
vitakapoondolewa.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema kuwa SADC inaamini katika ulinzi, usalama na
misingi bora ya kidemokrasia katika kutekeleza malengo yake, hivyo
masuala hayo ni ya msingi na ndiyo yatakayowezesha kuendeleza mikakati
waliyojiwekea.
Amesema
katika miaka 40 ya umoja na ushirikiano wao, wameweza kufanya mambo
makubwa ya maendeleo kwa nchi zao. “Miradi mbalimbali ya miundombinu
imeendelea kutekelezwa na tumeiwekea kipaumbele sekta ya viwanda ambayo
ni nguzo ya msingi katika kusaidia kukua kwa uchumi wa kanda na wa kila
mmoja wetu.”
Vilevile,
Waziri Mkuu amesema masuala ya kijamii kama elimu, afya, jinsia na
mazingira yameendelea kutekelezwa, ambapo alimnukuu Mwenyekiti wa SADC
Rais Dkt. John Pombe Magufuli, katika hotuba yake aliyoitoa wakati
anakabidhiwa Uenyekiti tarehe 17 Agosti 2019.
Alisema
“.....malengo ya umoja wetu kama yalivyoasisiwa na Wazee wetu wakati
SADC inaundwa, bado hatujayafikia, na iwapo juhudi za dhati na za pamoja
hazitachukuliwa, itachukua muda mrefu malengo haya kuyafikia....”.
Mwisho wa kunukuu.
Waziri
Mkuu amesema ni dhahiri kuwa wameendelea kupiga hatua kubwa hadi sasa,
lakini wanapaswa kuongeza kasi zaidi ya utekelezaji ili wahakikishe kuwa
malengo ya SADC yanafikiwa. “Changamoto tunazozipitia ni nyingi
ikiwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, tofauti za kisera na kimkakati
baina ya Nchi Wanachama, gharama za kufanya biashara na ushiriki hafifu
wa sekta binafsi.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema jumuiya hiyo kwa sasa iko katika maandalizi
ya kuwa na mkakati mpya wa utekelezaji wa yale yote wanayoazimia kwa
miaka kumi ijayo yaani mkakati wa mwaka 2020 hadi 2030.
Amesema
mkakati huo utahakikisha wanafikia malengo ya dira ya SADC ya miaka 30
ijayo kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2050. “Sote tunaamini kuwa mkakati
huu mpya tunaojiwekea utazingatia changamoto hizi na nyingine nyingi ili
kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.”
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuziomba na kuzisisitiza nchi wanachama
zishiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wanapata mikakati
inayotekelezeka na inayozingatia mahitaji ya kila mmoja wao na ya Kanda
kwa ujumla.
“Ni
matumaini yangu kwamba majadiliano na maazimio ya mkutano huu wa Baraza
la Mawaziri yataisogeza mbele Jumuiya yetu. Nimeona mna ajenda
muhimu mbele yenu kwa ajili ya mustakabali wa Jumuiya hii. Niwaombe
mzijadili kama inavyostahili na kutoa mwelekeo wa kisera ipasavyo.”
Kwa upande wake,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti
wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Profesa Palamagamba Kabudi amesema
mkutano huo unafanyika kwa njia ya mtandao kufuatia ushauri na
mapendekezo waliyoyapokea kutoka kwa Mawaziri wa Afya wa Nchi Wanachama
wa SADC walipokutana kwa dharura Dar es Salaam tarehe 9 Machi, 2020 kwa
ajili ya kujadili mlipuko wa corona.
Profesa
Kabudi amsema kupitia mikutano hiyo, Jumuiya imeendelea kuimarika kwa
kupitisha maazimio na mikakati mbalimbali itakayowezesha SADC kujizatiti
ipasavyo na kuleta mchango na maendeleo yanayotegemewa na nchi
wanachama.
“Nazishukuru nchi zote za SADC kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Sekretareti ya SADC na kwa Tanzania wakati waMaandalizi
ya Mikutano ya kisekta. Ni matumaini yangu kuwa maazimio na mikakati
iliyotokana na mikutano hiyo itasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.”
Amesema
pamoja na mafanikio hayo, SADC imeendelea kukumbana na changamoto
nyingi ikiwemomigogoro ya kisiasa, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya
asili, ukuaji wa idadi ya watu, ukuaji wa miji, elimu, afya, kupungua
kwa kasi ya uchumi, na masuala ya utawala. “Changamoto hizi siyo mpya na
kadri tunavyosonga mbele, kila mojawapo inakuwa ndiyo chachu ya
kuboresha maisha ya Wanajumuiya na hatimaye kuleta ustawi kwa wananchi
wetu.”
Awali,
Katibu Mkuu wa SADC, Bibi Stergomena Tax alizipongeza nchi wanachama wa
jumuiya hiyo kwa hatua mbalimbali walizozichukua katika kukabiliana na
mlipuko ugonjwa wa homa ya mapafu ulioikumba dunia ambao unaosababishwa
na virusi vya corona.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipunga mkono kuwaaga washiriki wa
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa
Afrika (SADC) baada ya kufungua mkutano huo kwa njia ya video kwenye
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es
salaam, Machi 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri
wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) kwa njia ya video
kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es
salaam, Machi 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia washiriki wa Mkutano wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) alioufungua
kwa njia ya video kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius
Nyerere jijini Dar es salaam, Machi 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...