VIJANA nchini wametakiwa kutokata tamaa ya maisha badala yake wawe wepesi wa kuchangamkia fursa pindi zinapojitokeza na siyo kukaa mitaani na kulalamikia ugumu wa maisha.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira, Mhe Anthony Mavunde wakati wa ufunguzi wa kongamano la vijana wakulima wilayani Butiama, Mara.

Mhe Mavunde amesema zaidi ya vijana 20,000 watanufaika na soko la  mazao ya matunda nchini kote  katika viwanda vilivyopo hapa nchini ikiwemo cha  Bakharesa ambapo yatatumika katika utengenezaji wa sharobati (Juice), hivyo kuwataka vijana hao kutokata tamaa.

Akiongea na vijana hao amesema mazungumzo yamefanyika baina ya Wizara yake na uongozi wa kiwanda cha  Bakharesa ili kuweza kununua matunda kama maembe  na ukwaju yanayozalishwa na vikundi vya vijana.

Amewataka vijana kutokata tamaa na kuwasisitizia kujiajiri katika fursa walizonazo zikiwemo ardhi ya kilimo  nguvu na afya bora walizobarikiwa  kwa kuwa tayari Serikali imeshaweka mazingira wezeshi kwa vijana kufanya kazi hiyo.

Mhe Mavunde amewataka vijana  hao kutumia kongamano hilo la siku mbili ili kupata mbinu mpya  na fursa za kilimo ufugaji na uvuvi ili kuweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Naibu Waziri Mavunde amesema ili kuhakikisha vijana wanapata mbinu bora za kilimo, Wizara yake itaendelea  kuendesha programu ya kuwapatia vijana ujuzi wa kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba (Green House).

"Programu hii inalenga kuzifikia Halmashauri zote nchini  ambapo kundi kubwa la vijana  litanufaika na mafunzo ya kilimo kupitia teknolojia hii ambapo jumla ya vijana 8,700 kutoka Halmashauri 84 za Mikoa 12 tayari wamepatiwa mafunzo ya kilimo kupitia teknolojia hiyo.

Nizitake Halmashauri zote nchini kutenga maeneo rafiki ya kilimo kwa ajili ya vijana kwa kuwa lilikuwa azimio  la Wakuu wa Mikoa la mwaka 2014 kuhusu kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana," Amesema Mavunde.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe Adam Malima akimkaribisha Naibu waziri huyo  amewataka Wadau kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya habari hasa mitandao ya kijamii kuwawezesha vijana kupata habari zinazofaa kuhusu kilimo lakini pia kuweza kufikia masoko kwa urahisi zaidi.

" Niwasihi pia kutumia mitandao ya kijamii vizuri, kule kuna fedha nyingi pia kama mtakua serious, kuna fursa nyingi yakiwemo masoko ya biashara yanapatikana kule, muhimu ni kuwa wabunifu na kuongeza jitihada," Amesema Mhe Malima.
 Baadhi ya vijana waliojitokeza kushiriki kongamano la siku mbili la vijana wakulima wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira, Mhe Anthony Mavunde wakati akizungumza nao kwenye ufunguzi wa kongamano hilo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira, Mhe Anthony Mavunde akizungumza na vijana waliojitokeza kwenye kongamano la vijana wakulima wilayani Butiama mkoani Mara.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...