SERIKALI imewataka wahitimu wa vyuo vya kilimo kote nchini kutumia fursa ya uhaba wa maafisa ugani ulioko nchini kwa kwenda kutoa elimu kwa wakulima na kuanzisha mashamba ya mfano  kwa wakulima

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kongamano la vijana wakulima mkoani Arusha, Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omari Mgumba amesema kwamba  maafisa ugani   wafungue mashamba ya mfano na watoe huduma kwa wakulima kama sehemu ya kujiajiri   .

“Sasa hivi kilimo kimebadilika wapo watu ambao wanazunguka kuwatafuta wataalamu  wa kilimo ili wakapate huduma kwenye shughuli zao na wapo tayari kulipia wataalamu  lakini wagani  hawapatikani," Amesema Mhe Mgumba.

Amewataka vijana kuwekeza kwenye  Uzalishaji wa mbegu bora za mazao nchini kwani kuna  uhitaji mkubwa wa mbegu nchini.

Akitolea mfano amebainisha kwamba  mahitaji ya mbegu ni tani 187,000 kwa mwaka wakati uzalishaji wa ndani ni tani 71,000  hivyo amewataka vijana kutumia fursa hiyo kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu hasa za mazao ya bustani na maua katika ukanda huuwa kaskazini ambao unajumuisha mikoa ya Arusha,Tanga,Kilimanjaro na Manyara.

Hata hivyo amebainisha kwamba jumla ya  vijana hapa nchini  ni milioni 16.1 sawa na asilimia 35 ya idadi ya watu wote, Kwa mujibu wa Utafiti wa Nguvu Kazi ya Taifa wa mwaka 2014, nguvu kazi ya vijana ni asilimia 67.1 ya  nguvu kazi yote ya Taifa na kiwango cha ukosefu wa ajira ni  asilimia 11.7 ya nguvu kazi yote.

“ Takwimu hizi zinaonesha umuhimu wa Nguvu Kazi ya Vijana na Sekta ya Kilimo kwa maendeleo ya Taifa” Amebainisha Mhe Mgumba.

Aidha  amesema kilimo ndio sekta pekee ambayo haibagui  mtu aliyesoma na asiyesoma kwani kilimo kinahitaji elimu kidogo sana na unapata utajiri kupitia kilimo alisisitiza Mhe. Mgumba.

 Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza Mkakati wa Miaka Mitano wa Taifa kwa Vijana kushiriki katika sekta ya kilimo wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21. Utekelezaji wa Mkakati huo unahusu masuala ya ardhi ya kilimo, rasilimali fedha kwa ajili ya kilimo, pembejeo na zana za kilimo, masoko ya mazao ya kilimo, mabadiliko ya tabianchi, ujasiliamali .

Hata hivyo alibainisha kwamba Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana ambapo tayari inatekeleza  Mkakati wa Kupunguza Upotevu wa Mazao Baada ya Kuvunwa na takwimu zinaonesha upotevu wa mazao yasiyo ya nafaka ni asilimia kati ya 30-40 ili kupunguza hasara kwa mkulima.

Aidha, Naibu Waziri amefafanua kwamba Wizara ya Kilimo kupitia TPRI  itaendelea kutoa mafunzo ya matumizi bora ya viuatilifu kwa wakulima na wafanyabiashara nchi nzima ili kuhakikisha matumizi bora ya viuatilifu na afya ya mimea ili kumsaidia mkulima.

“TPRI imeendelea kusajili viuatilifu, kufanya ukaguzi wa pembejeo zisizofaa kwa matumizi ya kilimo kwa wafanyabiashara wasiowaaminifu na kutoa elimu kwa wakulima ili wasipate hasara za kutumia viuatilifu visivyo na ubora” Amesema Mhe. Mgumba
 Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omari Mgumba akikagua bidhaa za sola power kutoka  kampuni ya Poa Portable Power wakati wa kongamano la vijana lililofanyika Mkoani Arusha kushoto ni muoneshaji bwana Emanuel Godwin wa kampuni hiyo.
 Vijana ambao wameshiriki kongamano la Vijana wakulima mkoani Arusha wakimsikiliza Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba (hayupo pichani).
 Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba akizungumza kwenye kongamano la Vijana wakulima mkoani Arusha.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...