Na.Vero Ignatus,Arusha.
Mkoa wa Arusha umeona umuhimu wa kuanzisha utaratibu wa kuchukua sampuli na kuwapima madereva wa Malori yanayopita mpaka wa Namanga mkoani Arusha wakitokea nchi jirani ya Kenya kufuatia kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Mkuu wa mkoa huo Mrisho Gambo amesema kuwa Sampuli zote zinazochukuliwa na wataalam wa Afya zimekuwa zinapelekwa Maabara kuu ya Taifa Dar es Salaam kwa ajili ya kupata majibu ya vipimo husika.
Tumechukua uamuzi huu ili kuwalinda wananchi wetu na maambukizi ya COVID-19 kutoka nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa afya ya wananchi wetu kama sehemu ya maandalizi ya kupokea Watalii msimu utakapoanza mwezi Juni 2020.
Gambo alisema kuwa utaratibu wa kuchukua Sampuli za COVID-19 kwa Madereva wanaotoka Nchini Kenya ulianza kutumika tarehe 14/5/2020 na sampuli zilichukuliwa kuanzia tarehe 14,16 na 18 Mei 2020
Aidha matokeo ya maabara ni kama ifuatavyo: 1. Madereva 44 toka Kenya walichukuliwa vipimo tarehe 14/5/2020 na majibu yalitoka tarehe 16 Mei 2020 na matokeo ya vipimo ni kuwa madereva 14 (11 Wakenya, 1 Mganda na 2 kutoka nchi ambayo tunaihifadhi) kutoka upande wa Kenya walikuwa "Positive" na 30 walikuwa "Negative". 2. Tarehe 16/5/2020 Madereva 23 toka Kenya walichukuliwa vipimo na tarehe 19/5/2020 majibu yalikuwa 10 ni "Positive" (wote kutoka nchi ya Kenya) na 13 ni "Negative". 3.
Tarehe 18/5/2020 Madereva 11 kutoka Kenya walichukuliwa vipimo na majibu yatatangazwa mara baada ya kupatikana kutoka Maabara Kuu ya Taifa Dar Es Salaam. Aidha, ili kujiridhisha tulichukua upya Sampuli ya baadhi ya Madereva (Sampuli zilichukuliwa kwa Madereva 19) waliotoka Tanzania na kupimwa Mpakani Namanga upande wa Kenya na kutangazwa na nchi ya Kenya kuwa ni "Positive". Sampuli hizi baada ya kupelekwa maabara kuu ya Taifa Dar Es Salaam zilionyesha kuwa madereva hao waliotoka Tanzania ni "Negative"
Gambo alisema kuwa mkoa wa Arusha umejiridhisha kuwa hizi ni mbinu za nchi ya Kenya ili kuua Soko la Utalii Mkoani Arusha na Tanzania kwa Ujumla. Madereva wanao onekana kuwa ni "Positive" hawaruhusiwi kuvuka mpaka kuingia Tanzania wala kwenda Kenya. Mkoa wa Arusha unaendelea kuchukua tahadhari na kudhibiti maambukizi ya Covid-19 kupitia mpaka wa Namanga jirani na Nchi ya Kenya. Tunaendelea kushukuru kwa ushirikiano tunaoupata kutoka kwa majirani zetu Wakenya mpakani Namanga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...