Charles James, Michuzi TV

WATANZANIA wametakiwa kujiwekea Utamaduni wa kunywa maziwa kwa wingi na siyo kusubiri mpaka waandikiwe na Daktari kwani unywaji wa maziwa hujenga afya.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi leo wakati wa ziara yake ya kugawa maziwa kwa watu wenye mahitaji kwa kushirikiana na Bodi ya Maziwa ambapo wamegawa maziwa Lita 1650 yenye thamani ya Sh Milioni Nane.

DC Katambi amesema Ofisi yake itaendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa pamoja na kutoa elimu kwa wananchi huku akiagiza maziwa yanayogaiwa yawafikie walengwa.

Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, DC Katambi amewataka madaktari wa Hospitali hiyo kuhakikisha maziwa hayo yanawafiki walengwa ambao ni wagonjwa hasa akina Mama na watoto.

" Ndugu zangu hii ni wiki ya maziwa niwasihi tusiishie kunywa maziwa wiki hii tu, tuweke utaratibu wa kunywa maziwa kwa sababu yanachangia uimara wa mwili na ni kinga ya magonjwa.

Kunyweni maziwa kwa wingi na mimi kwenye Wilaya yangu nitahamasisha unywaji wa maziwa kwenye shule zetu, makazini na hata majumbani," Amesema DC Katambi.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa Dk Sophia Mrote amesema moja ya kazi ya wiki hii ya maziwa ni pamoja na kugawa maziwa kwa watu wenye uhitaji ambapo leo wamegawa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma, Kituo cha Afya Mkonze na vituo vya watoto wenye uhitaji cha Kijiji cha Matumaini na Kisedeti.

" Tunafuraha kuungana na nyinyi leo lakini tuwaombe mhamasishane kunywa maziwa hata baada ya wiki ya maziwa kuisha basi tuendelee kunywa kwa ajili ya kujenga afya zetu.

Niwapongeze makampuni yote ambayo yameungana na sisi hapa Dodoma kwenye ugawaji huu, hakika wameonesha uzalendo mkubwa na sisi kama Bodi ya Maziwa tunaahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuhamasisha unywaji wa maziwa," Amesema Dk Sophia.

Nae Meneja Masoko wa Kampuni ya Maziwa ya Tanga Fresh, Ally Sechonge amesema wao kama wadau wa maziwa hawatosita kushirikiana na serikali katika kuhamasisha unywaji wa maziwa pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida ya unywaji wa maziwa.

Licha ya kuchangia maziwa pia Kampuni hiyo imekabidhi vifaa vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na ugonjwa huo.

" Tuwasihi wananchi kuwa na utaratibu wa unywaji maziwa katika kuimarisha afya zao, sisi kama wadau tutaendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa kuanzia ngazi ya familia na pia kwenye shule," Amesema Sechonge.
 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi (mwenye suti katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote (kulia kwake) na watoa huduma wa afya Hospitali ya Rufaa Dodoma walipofika kugawa maziwa hospitalini hapo.
 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akizungumza na watoto wenye uhitaji wanaolelewa kwenye Kituo cha Kijiji cha Matumaini alipofika kituoni hapo kugawa maziwa kwa kushirikiana na Bodi ya Maziwa na Kampuni mbalimbali za Maziwa.
 Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote akionesha ndoo ya kunawia mikono kwa maji tiririka iliyotolewa na Kampuni ya Tanga Fresh kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Corona katika Kituo cha watoto wenye uhitaji cha Kijiji cha Matumaini leo.
 Meneja Masoko wa Kampuni ya Tanga Fresh, Ally Sechonge akigawa maziwa kwa mmoja wa watoto wenye uhitaji anaelelewa kwenye Kituo cha Kisedeti jijini Dodoma leo ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya maziwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...