Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)  akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Singida (hawapo pichani)  mara baada ya kupokea taarifa ya Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo hicho kuhusu Mkakati wa Uendeshaji Mafunzo kwa Kuzingatia Tahadhari Dhidi ya Maambukizi ya Corona, utakaoanza kutekelezwa na Chuo hicho pindi kitakapofunguliwa tarehe 01/06/2020.
Baadhi ya watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Singida wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (hayupo pichani) mara baada ya Naibu Waziri huyo kupokea taarifa ya Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo hicho kuhusu Mkakati wa Uendeshaji Mafunzo kwa Kuzingatia Tahadhari Dhidi ya Maambukizi ya Corona.
Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Emmanuel Shindika akimshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa kukitembelea Chuo cha Utumishi wa Umma ili kujiridhisha na mkakati wa Chuo hicho katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona (COVID 19), kabla ya chuo hicho kufunguliwa tarehe 01/06/2020.
Fundi Bomba aliyepewa jukumu la kutengeneza mabomba ya maji tiririka nje ya geti la Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida ili kuwawezesha wafanyakazi, wanafunzi na wadau wa chuo kunawa mikono yao na sabuni kwa maji tiririka.


James K. Mwanamyoto-Singida



Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kimepongezwa kwa kuunda vikosi kazi katika Kampasi zake vitakavyokuwa na jukumu la kusimamia shughuli za uelimishaji wanachuo dhidi ya ugonjwa wa Corona (COVID 19) na kushughulikia dharura zitakazojitokeza kutokana na ugonjwa huo, ikiwa ni sehemu ya mkakati mahususi katika kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye hivi karibuni alizitaka Taasisi za Elimu nchini kupokea wanafunzi na kuanza kutoa mafunzo ifikipo tarehe 01 Juni, 2020.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa katika ziara ya kikazi Kampasi ya Singida, mara baada ya kupokea taarifa ya Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma kuhusu Mkakati wa Uendeshaji Mafunzo kwa Kuzingatia Tahadhari Dhidi ya Maambukizi ya Corona, utakaoanza kutekelezwa na Chuo hicho pindi kitakapofunguliwa tarehe 01/06/2020.

Mhe. Dkt Mwanjelwa amefurahishwa na mpango uliowekwa na Chuo, kwa kila mwalimu anayeingia darasani kuhakikisha kabla hajaanza kufundisha kutoa elimu juu ya namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya COVID 19 ili kuwapa uelewa na kuondoa hofu kwa wanafunzi dhidi ya ugonjwa huo.

Dkt. Mwanjelwa ameridhishwa na jitihada za Chuo kuweka mabomba ya maji tiririka nje ya geti ili kuwawezesha wafanyakazi, wanafunzi na wadau wa chuo kunawa mikono yao na sabuni kwa maji tiririka ambapo walinzi getini watakuwa wakisimamia zoezi hilo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Emmanuel Shindika amemueleza Dkt. Mwanjelwa kuwa, licha ya vikosi kazi hivyo kuwa na jukumu la kuelimisha wanachuo kuhusu ugonjwa wa Corona na kushughulikia dharura zitakazojitokeza, pia vitakuwa na jukumu la kukagua miundo mbinu na vitendea kazi ili kujiridhisha na ubora wake ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na uwepo wa maji tiririka ya bomba na sabuni ya kusafisha mikono.

Aidha, Dkt. Shindika amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa kukitembelea Chuo cha Utumishi wa Umma ili kujiridhisha na mkakati wa Chuo hicho katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona (COVID 19), kabla ya chuo hicho kufunguliwa tarehe 01/06/2020.

Mnamo tarehe 21 Mei, 2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alitangaza kufunguliwa kwa vyuo vyote nchini ifikapo tarehe 01 Juni, 2020 hivyo Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kilifanya tathmini na kuainisha maeneo hatarishi kwa maambukizi ya Virusi vya COVID-19 na hatimaye kuandaa Mkakati Madhubuti wa Uendeshaji wa Mafunzo kwa Kuzingatia Tahadhari Dhidi ya Maambukizi ya Ugonjwa wa Corona (COVID-19).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...