Na Mwandishi Mwandishi Wetu.

UHURU wa kutoa maoni, kujieleza na kupata taarifa ni mojawapo wa Haki za Msingi za raia wa Tanzania kama ilivyosisitizwa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo upo mkanganyiko katika kutafsiri maana ya Uhuru huu  uliojikita zaidi katika kukidhi matakwa na maslahi fulani.

Kwa upande mmoja, wapo wanaotafsiri dhana ya uhuru wa kutoa maoni na kujieleza kama Haki ya raia yeyote kuwasilisha mawazo na fikra zake bila vikwazo. Wanaoamini katika dhana hii huchagiza kuwapo kwa mazingira wezeshi kwa raia kutoa mawazo yao, kuhoji, kupewa na kutoa taarifa zinazohusu mustakbali wa maisha yao.

Kwa upande mwingine wapo wanaoamini kwamba Uhuru wa kutoa maoni, kujieleza na kupata taarifa ni Haki ya kikatiba ingawa utekelezaji wa Uhuru huu unaenda sambamba na uwajibikaji. Mantiki ni kwamba, katika kutekeleza Uhuru huu kila raia anao wajibu wa kuhakikisha haathiri au kuhatarisha Uhuru wa raia mwingine ambao pia unalindwa kikatiba.

Changamoto za uelewa wa Uhuru wa kutoa maoni na kujieleza.
Ingawa tafsiri za makundi yote mawili zinahimiza kutimizwa kwa Haki hizo za msingi za kiraia, bado zina mapungufu katika utekelezaji wake. Kwanza, hauwezi kuwa na Uhuru usiokuwa na vikwazo katika mambo ya msingi, mfano afya (uhai) ya jamii, ulinzi, usalama na haki ya kujisitiri. Raia wanayo haki ya kuelimishwa kwamba uhuru wa kutoa maoni na kupata habari hauhusishi, kwa mfano, kuelezwa au kutoa maoni kuhusu idadi ya wanajeshi, silaha au taarifa zinazohatarisha usalama wa nchi na afya ya raia kwa ujumla.

Elimu zaidi itolewe kwa wananchi kwamba Uhuru wa kutoa maoni na kujieleza haumaniishi kutamka chochote, kwa yeyote, wakati wowote na mahali popote, la hasha! Bahati mbaya baadhi ya raia wanautumia vibaya Uhuru kupitia mitandao ya kijamii kwa kuwachafua wengine na kutoa taarifa za upotoshaji. Ni wajibu wa kila raia kuutumia Uhuru na Haki ya kujieleza kwa busara ili kuepusha migogoro katika jamii.

Pili, hauwezi kuweka vikwazo vingi vya kisheria na kikanuni ili kudhibiti Uhuru wa raia kutoa maoni na kujieleza kwa utetezi wa kuimarisha uwajibikaji. Udhibiti wa Uhuru wa kutoa maoni husasan wenye mlengo wa kuhoji na kukosoa mawazo fulani, sera au utendaji fulani umetekelezwa na nchi nyingi barani Afrika kwa kisingizio cha kulinda maslahi ya nchi.

Sheria mbalimbali zinazohusu utoaji na upashanaji taarifa zimejielekeza katika kudhibiti utoaji na upatikanaji wa taarifa hizo kupitia vyanzo tofauti. Mfano Asasi za Kiraia, Kwa Tanzania Taasisi za Habari na Mashirika yasiyo ya Serikali kama vile MCT, MISA- Tan, THDRC na LHRC na mengine mengi yamekuwa yakipaza sauti kutaka kupitiwa upya ili kuboreshwa sheria mbalimbali zenye vipengele vinavyokandamiza Uhuru wa kujieleza na kupata taarifa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) ya mwaka 2018 utekelezaji wa Sheria kama vile Sheria ya Takwimu (2015), Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (2016) na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni (2015)  umeongeza shinikizo na hofu miongoni mwa Vyombo vya Habari na wananchi kujiwekea vikwazo kutoa taarifa hasa zile zinazokinzana na mamlaka.

Nini kifanyike?
Kujenga uelewa sahihi kwa wananchi kuhusu maana na umuhimu wa Uhuru wa kutoa mawazo na kujieleza ili kuwawezesha kuitumia ipasavyo haki yao ya kikatiba kuchangia mawazo, kuhoji, kukosoa ama kukosolewa kuhusu jambo lenye maslahi mapana kwa jamii.

Kuwepo kwa mazingira wezeshi ikiwemo kufanya marekebisho ya Sheria zisizo rafiki kwa raia kutoa maoni yao na kujieleza kwa njia sahihi ikiwemo kuhoji utendaji wa viongozi wao katika mchakato wa maendeleo ya Nchi na wananchi kwa ujumla.

Kwa kuwa kumekuwa na matukio ya kukamatwa raia kwa makosa ya kimtandao, ipo haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika kutoa na kupata taarifa pasipo kujihusisha na upotoshaji wa aina yoyote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...