MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na taasisi mbili zisizo za serikali waliokuwa wakipinga marekebisho katika Sheria ya Makampuni Sura ya 212, Sheria ya Asasi Zisizo za Serikali Sura ya 337 na Sheria ya Usajili wa Wadhamini Sura ya 318.

Marekebisho katika sheria hizo yalihusu  kuweka tafsiri mpya ya maneno Kampuni na Asasi katika sheria husika na pia kuzitaka Asasi zote zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni ambazo hazikuwa na malengo ya kibiashara  kujisajili chini ya sheria na iwapo zingeshindwa kufanya hivyo ndani ya muda wa miezi miwili zingehesabika kuwa zimefutiwa usajili wake.

Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 21/2019 ilifunguliwa na 29 Agosti, 29, 2019 na Taasasi isiyo ya kiserikali ya Centre for Strategic Litigation inayomilikiwa na Wakili wa Kujitegemea Jebra Kambole pamoja na Asasi ya Change Tanzania Limited inayomilikiwa na Maria Sarungi.

Akisoma uamuzi huo,  Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Lameck Mlacha akisaidiana na Jaji Yose  Mlyambina na Stephen Murimi Magoiga, alisema waleta maombi wameshindwa kuleta hoja za msingi kutetea maombi yao.

Hivyo, alisema analitupilia mbali shauri hilo na kuelekeza taasisi hizo kulipa gharama za uendeshaji wa shauri hilo kwa serikali.

Katika hoja za serikali ilipinga maombi hayo kwa hoja mbalimbali ikiwemo  walalamikaji wameshindwa kubainisha na kuithibitishia mahakama athari ambazo zinatokana na marekebisho hayo ya sheria kwa kiwango kinachostahili katika mashauri ya Kikatiba.

Ilidai maombi yaliyowasilishwa mahakamani yaliegemea zaidi katika hisia za walalamikaji na sio maslahi mapana ya umma.

Katika maombi yao, asasi hizo zilipinga marekebisho ya Sheria husika kwa msingi kuwa yalikiuka ibara za 13(1), (2), (6)(a),(b); 20(1) na 29(1) na (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kile kilichodaiwa kuwa marekebisho hayo yanakinzana na haki ya usawa mbele ya sheria, uhuru wa kujumuika na haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...