Na Nyamiti Kayora

Kwa miaka zaidi ya 30 Margreth Ibrahimu, mama wa watoto 7, amekuwa akitumia kuni kupikia na mara chache sana mkaa.

Kijiji cha Mindutulieni kilichopo kata ya Lugoba, wilayani Chalinze Mkoani Pwani anachokaa Magreth tangua kuanzishwa kwake mwaka 1980 hakijawahi kuwa na nishati nyingine ya kupikia zaidi ya kuni na mkaa.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati Tanzania Bara ya mwaka 2016 inaonesha kuwa kaya 7 kati ya kumi mkoani Pwani zinatumia kuni na mkaa kama chanzo cha nishati ya kupikia.

Licha ya kuwa na mifugo lukuki na kinyesi cha mifugo yao kuwa ni nishati muhimu katika kuzalisha gesi ya kupikia na mwanga, wanakijiji hawa hawatumii hata kidogo kinyesi hicho kuzalisha nishati.

Magreth, ambaye anamiliki ng'ombe 10, anasema kwake anatumia Kuni kupikia, kwa kuwa upatikanaji wake ni wa haraka na rahisi na amekuwa akitumia nishati hiyo tangu akiwa mtoto.

“Tumezaliwa, wazazi wetu wanatumia (kuni) nami nimeolewa naendelea kutumia kuni kupikia," alisema Magreth. Siyo Magreth tuu anayetumia kuni kama nishati ya kupikia, bali hata Sara Kasha aliyeenzi utamaduni huo toka kwa wazazi wake na jamii yake ya kifugaji.

Sara anasema yeye kuni huokota katika maeno yake ya jirani na endapo huitaji kutumia mkaa pia upatikanaji wake ni nafuu kulingana na mazingira ya kijiji chao kilicho na miti mingi.

“Sisi tushazoea kutumia kuni, kwanza huku pori kubwa tunaokota tu na tukitaka kutumia mkaa tunakata miti tunachoma au tunanunua kwa wachomaji,” alisema Sara.

Wanakijiji hapa Mindutulieni wanatumia nishati hii ya kuni licha ya wilaya ya Chalinze kuwa na majiko sanifu jambo linalotokana na elimu ndogo kuhusu nishati ya kupikia ikiwemo matumizi ya gesi.

"Kweli mimi natamani kutumia gesi ila ndo sijui inatumiwaje, mafundisho hatujapata hata kuulizia tuu bei yake dukani tunaona shida,” alisema Sara.

Wakati wengine wakiwa hawana elimu ya matumizi ya gesi au majiko sanifu, baadhi wanasema hawawezi kuyamudu kutokana na umaskini uliowakithiri.

“Uwezo wetu wa kifedha ni kipato cha chini. Huwezi kupata hela ukaenda kununua jiko la gesi ambalo gharama yake ni kubwa na wakati huo una mahitaji mengi katika familia,” alisema Veronica Katei.

Kiutamaduni wanawake ndiyo hushughulika kwa kiasi kikubwa na masuala ya jikoni na tafiti nyingi zinaangazia suala hili katika jicho la kijinsia na namna ambavyo mwanamke amekuwa akitumia muda wake mwingi kusaka kuni kwa umbali mrefu.

HATARI YA MATUMIZI KUNI

Licha ya kutumia nishati hii wanawake hawa wanaowakilisha wenzao zaidi ya 500 kijijini hapa, Sara Kasha anasema utumiaji wa kuni umekuwa ukiwapatia matatizo ya kiafya.

“Upikaji wa kuni unatuathiri maana hata shuleni tulifundishwa moshi unaharibu macho, na kuna wakati tunabanwa kifua, lakini bado tunatumia maana hatuna jinsi,” aliongeza Sara.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa matumizi makubwa ya kuni yanaweza kusababisha madhara ya muda mrefu ya kiafya kama anavyoeleza Dkt. Frank Sandi ambaye ni mkufunzi katika chuo kikuu cha Dodoma Idara ya Afya katika kitengo cha macho.

“Kwa mtumiaji wa kuni hawezi kupata madhara ya haraka au ya moja kwa moja, Hivyo ule moshi humuathiri taratibu mtumiaji,” alisema.

Pia Dkt. Sandi amebainisha kuwa endapo mtu anakuwa na tatizo la macho ama mzio, utumiaji wa kuni uendelea kumuathiri zaidi na yule anayetumia kwa muda mfupi na kuacha kisha kurejea tena kutumia kuni anaweza pata madhara zaidi.

“Mtu mwenye mzio, ama matatizo mengine ya macho akitumia kuni ule moshi utaendela kumuathiri zaidi hasa pale atakapokuwa anapikicha macho yanazidi kuathirika,” aliongeza.

Vilevile Dkt. Sandi amebainisha kuwa utumiaji wa moshi pia unaweza leta athari kwa kifua kubana hasa kwa watu wenye matatizo ya pumu.

“Kuna watu wanabanwa kifua wakipata moshi wa kuni, na wengi ni wale wenye ugonjwa wa pumu hivyo ni bora mtu mwenye tatizo hilo asitumie ili kuilinda afya yake,”aliongeza.

Hata hivyo jitihada nyingi zimechukuliwa katika kuhakikisha serikali kwa kushirikiana na wadau wa nishati wanaungana kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu ikiwemo nishati ya umemejua, umeme utakaona na vinyesi vya wanyama (bayogesi) unaoleta tija kwa matumizi ya kupikia hasa katika maeneo ya vijijini.

Ingawa ili wafugaji waweze kupata nishati ya kupikia kama wakazi wa Mindutulieni itokanayo na vinyesi vya wanyama (bayogesi) ni lazima elimu ya namna ya kutengeneza nishati hiyo iwafikie wananchi husika.

Mbali na elimu, inabainishwa pia ufugaji wao uwe wa kuwafungia eneo moja kama anavyoeleza Sisty Basil, Mkurugenzi wa Taasisi ya ELICO inayojihusisha na usambazaji wa umeme jua iliyopo jijini Dar es Salam.

Sisty anasema ili mfugaji aweze kupata bayogesi ni lazima ufugaji wake uwe wa kitaalamu usiohusisha kuhamahama na vyanzo vya mapato vitakavyosaidia uwekezaji wa gesi hiyo asilia.

“Kwanza kuwepo na mtaji wa kutosha katika uwekezaji, pili wananchi wapatiwe elimu ya utengenezaji wa bayogesi pamoja na ufugaji wa kisasa, ili upatikanaji wa kinyesi uwe eneo maalam,” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...